Farida Mangube, Morogoro
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, ametoa wito kwa wananchi na taasisi zote kuhakikisha wanazingatia ubora wa vipimo katika shughuli zao za kila siku, akisisitiza kuwa vipimo visivyo sahihi vinaweza kuathiri afya, usalama, haki katika biashara, na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
DC Kilakala alitoa kauli hiyo Mei 20, kwenye Maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Morogoro, ambapo amsema vipimo sahihi ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisayansi.
“Tunapoadhimisha Siku ya Vipimo Duniani, ni wajibu wetu kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika shughuli zetu za kila siku vinakidhi viwango vya kimataifa.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, amesema kuwa uhakiki wa usahihi wa vipimo katika sekta kama viwanda, afya, ujenzi, na usafiri wa anga ni hatua muhimu ya kuhakikisha bidhaa na huduma zinazotolewa zina ubora unaostahili na zinawalinda watumiaji.
“Vipimo vikihakikiwa kwa usahihi wake vitaleta manufaa makubwa kwa jamii,” alisema Dkt. Katunzi.
“Vitawezesha utoaji wa huduma bora na bidhaa zenye ubora katika sekta kama afya, mawasiliano, chakula, na nyingine nyingi.”
Aidha, amesema Tanzania, kupitia maabara ya TBS, imekuwa nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki kupata ithibati ya kimataifa katika vipimo vya torque, barometa na unyevu — hatua inayoiwezesha kutoa huduma za ulinganifu wa vipimo kwa kiwango cha kimataifa.
Katika maadhimisho hayo TBS imewakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali za umma na binafsi ambapo Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Vipimo kwa Nyakati Zote na kwa Watu Wote”, ikisisitiza umuhimu wa vipimo sahihi katika kuchangia maendeleo endelevu na ustawi wa jamii katika nyanja zote za maisha.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...