Na WMJJWM- Mwanza.
KATIBU  Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amewataka Wataalam wa Sayansi ya Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kutumia teknolojia katika kutatua changamoto za Malezi na kuboresha Sayansi ya Malezi kwa watoto.

Dkt. Jingu amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Malezi na Mkuzi ya Awali ya mtoto linalofanyika kuanzia Mei 23-24, 2025, katika ukumbi wa Rocky City mall Jijini Mwanza.

Dkt. Jingu amesema kumekuwa na ombwe kati ya kizazi cha zamani na cha sasa katika suala la malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto hivyo kama Wataalam watatumia teknolojia vizuri itasaidia kuondoa ombwe hilo na kutatua changamoto zilizopo katika Malezi nchini.

"Sisi wote tulivyo leo ni kwa sababu ya malezi tuliyopata kutoka kwa wazazi wetu, hivyo ni muhimu na sisi kuendeleza dhamira ya malezi bora kwa watoto ili kuwa na Taifa imara na lenye maadili mema" amesema Dkt Jingu.

Aidha Dkt. Jingu ameongeza kwamba katika wakati huu ambapo Maendeleo ya TEHAMA yamechukua nafasi kubwa katika Jamii amewaasa Wataalam wa Malezi kutumia Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kuhakikisha Jamii inapata elimu ya malezi kwa watoto.

"Tunaweza kuwa na Majukwaa ya wazazi katika mitandao ya kujadiliana kuhusu Malezi na changamoto zilizopo katika kuzipatia ufumbuzi hata kuwa na Majukwaa kwa watoto yatakayotoa elimu,burudani na michezo kwao yenye kuzingatia maadili yetu" amesisitiza Dkt. Jingu

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Baladya Elikana amesema suala la malezi ni muhimu kuzingatiwa hasa katika kujenga taifa lenye watu wenye maadili na uzalendo kwa nchi yao.

"Najua lengo la kongamano hili ni kutathmini utekelezaji wa programu mbalimbali za malezi katika jamii na kutoa utatuzi wa changamoto mbalimbali za malezi na makuzi katika jamii hivyo tutumie Kongamano hili kuleta mabadiliko katika suala Malezi kwa watoto wetu." amesema Elikana

Kongamano la melezi ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya familia ambayo huadhimishwa Mei 15 kila Mwaka. Kongamano hilo limewakutanisha Wataalam wa malezi, Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii na wadau kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayotoa Huduma za malezi kwa watoto pamoja na Watafiti wa malezi kutoka Taasisi za Elimu ikiwemo Chuo Cha Utafiti Ifakara, Chuo cha Ustawi wa Jamii, na Chuo Kikuu cha Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...