Na Mwandishi Wetu, Malunde 1 blog


Mbunge wa Jimbo la Msalala mkoani Shinyanga, Mhe. Iddi Kassim, ametoa baiskeli 92 kwa wenyeviti wa vijiji vyote vya Halmashauri ya Msalala kwa lengo la kuwawezesha kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.


Baiskeli hizo zenye thamani ya shilingi milioni 23 zimekabidhiwa rasmi katika hafla iliyofanyika leo katika kata ya Bugarama zikiwa ni kwa ajili ya wenyeviti wa vijiji katika jimbo zima la Msalala kwa lengo la kurahisisha usafiri wa viongozi hao kuzungukia miradi ya maendeleo katika maeneo yao.


Zoezi hilo la ugawaji wa baiskeli limefanyika leo Mei 4,2025 likiongozwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa, Mohammed Ali Kawaida, ambaye pia amehutubia wananchi na kuwahimiza kuhakikisha miradi ya maendeleo inalindwa na kutunzwa kwa manufaa ya wote.


“Ni jambo la kuigwa. Mbunge amewawezesha viongozi wa msingi kufanikisha usimamizi wa maendeleo ya wananchi. Nawasihi wenyeviti kutumia baiskeli hizi kwa shughuli zilizokusudiwa,” amesema Kawaida na kupongeza hatua hiyo aliyoitaja kuwa ya kipekee katika ziara yake ya siku 10 nchini.


"Naomba mkazitunze hizi baiskeli ili ziwasaidie katika kuzungukia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na ilani ya Chama cha mapinduzi (CCM)", amesema.



Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge Iddi amesema kuwa wenyeviti wa vitongoji na vijiji wanafanya kazi kubwa bila kuwa na mshahara na kwamba jimbo la msalala lina utajiri mkubwa unaoweza kuwapa posho wenyeviti hao kupitia mapato ya ndani.


Ameeleza kuwa kila baiskeli imegharimu shilingi 250,000, na kwamba hatua hiyo inalenga kuwawezesha wenyeviti kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kuhakikisha changamoto zinagunduliwa mapema na kutafutiwa ufumbuzi.


Aidha Mheshimiwa Iddi amewataka viongozi kuwatumikia wananchi kwa kusimamia kwa uaminifu miradi ya maendeleo ili kuinua Uchumi wa taifa na Uchumi wa mtu mmoja mmoja.


“Katika vijiji vyetu, kuna miradi mingi inayoendelea na inahitaji usimamizi wa karibu. Nitashirikiana na viongozi hawa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo ya kweli,” ameongeza.


Wakizungumza mara baada ya kupokea baiskeli hizo baadhi ya wenyeviti wamemshukuru Mbunge Iddi na kwamba baiskeli hizo zitawasaidia katika majukumu yao.


Katika tukio hilo, wanachama tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoka Wilaya ya Kahama, wakiongozwa na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Tendaji ya wilaya hiyo, Samson Thomas, wamehamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupokelewa rasmi na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa.


Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Thomas amesema wameamua kuunga mkono juhudi za serikali ya CCM katika kusukuma mbele maendeleo ya wananchi, na kuahidi kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama na uongozi, huku akiahidi kuwa mtiifu kwa chama hicho.


















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...