MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali inalaani vikali na kukemea tukio la kushambuliwa na kuumizwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Padre Dkt. Charles Kitima pamoja na matukio mengine kama hayo ya uvunjifu wa sheria.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati aliposhiriki katika Misa ya Kumsimika Askofu wa Jimbo Jipya Katoliki la Bagamoyo Mhashamu Askofu Stephano Lameck Musomba pamoja na Sherehe ya Uzinduzi wa Jimbo hilo iliyofanyika katika Uwanja wa St. Mary Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani. Amewahakikishia Watanzania na wapenda haki, amani na usalama, kuwa tayari Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani imeviagiza vyombo vya dola kuwatafuta, kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika wa tukio hilo, na wale wote watakaothibitika kuhusika na matukio kama hayo.
Aidha Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu wakati wote wa maandalizi na kampeni za uchaguzi mkuu. Amesema ni vema kuepuka kauli za kibaguzi, kichochezi, uzushi na upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii na njia nyingine za mawasiliano kwa misingi ya tofauti ya itikadi za kisiasa, kidini, kabila au rangi.
Vilevile Makamu wa Rais amewaasa vijana kutokubali kutumiwa na wanasiasa wenye uchu wa madaraka, walio tayari kuwatumia kuchochea vurugu wakati wa uchaguzi kwa manufaa yao wenyewe. Amewasisitiza watendaji Serikalini kutenda haki katika utekelezaji wa majukumu waliyokabidhiwa. Pia amesema ni muhimu kuendelea kuliombea Taifa letu kwa Mwenyezi Mungu ili liwe na amani na utulivu, hususan mwaka huu tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wa dini na taasisi zake ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kuhudumia umma wa watanzania. Ameongeza kwamba Serikali inathamini mchango mkubwa wa Kanisa Katoliki na madhehebu mengine ya dini katika kuimarisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za jamii, hususan afya na elimu.
Amesema uamuzi wa hayati Baba Mtakatifu Francis kuunda Jimbo jipya la Bagamoyo, si tu umeipa Bagamoyo hadhi, lakini pia umesogeza huduma za kichungaji kwa waamini na utaongeza kasi ya uinjilishaji.
Makamu wa Rais amewasilisha salamu na pongezi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wanajimbo la Bagamoyo kwa kupata Jimbo na Mchungaji Mkuu. Amesema Bagamoyo imekuwa ndiyo mlango wa kuingia kwa imani ya kikristo hapa nchini na maeneo mengine ya Afrika Mashariki na Kati.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...