Na John Mapepele
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtaka Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia eneo la Afya katika Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Prof. Tumaini Nagu kuhakikisha kwamba huduma ya afya ya msingi inaboreshwa kwa wananchi.
Mhe. Rais ametoa maelekezo hayo leo, Mei 24, 2025 Ikulu ya Dar es Salaam mara baada ya kumuapisha kushika washifa huu baada ya kumteua hivi karibuni.
Mhe. Rais amefafanua kwamba tayari Serikali imeshafanya maboresho makubwa katika eneo hili kazi iliyobaki ni kuendelea kusimamia kikamilifu ili kuimarisha eneo hili.
" Toka mwaka 2020 Serikali imefanya mambo makubwa katika eneo hili kuanzia kwenye ukarabati wa zahanati kongwe, vituo vya afya, ongezeko la vifaa tiba na wataalam". Amesisitiza Mhe. Rais
Pia Mhe.Rais amemtaka Profesa Nagu kwa kushirikiana na viongozi atakaowakuta kwenda kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wananchi kwenye sekta hiyo muhimu kwa taifa letu.
Aidha, amemtaka katika utendaji wa kazi kupunguza urasimu huku akizingatia miongozo, sheria na kanuni katika utendaji wa kazi.
Katika uapisho huo, Waziri wa Ofisi ya Rais- TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa, Katibu Mkuu, Adolf Ndunguru na Watendaji kadhaa wa Wizara pia wameshiriki.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...