Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema Serikali imefikisha umeme kwenye mitaa 58 ya Mji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kati ya mitaa 81 ya Halmashauri hiyo.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Mei 26, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Tarime Mjini, Mhe. Michael Kembaki aliyeuliza Serikali itapeleka lini umeme katika mitaa 18 ya Halmashauri ya Mji wa Tarime.
"Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime ina mitaa 81, kati ya hiyo mitaa 58 tayari imefikiwa na umeme, na mitaa 23 bado haijafikiwa na umeme." Amesema Kapinga
Ameongeza kuwa, mitaa 13 inapelekewa umeme kupitia mradi wa Hamlets Electrification Project - IIA (HEP IIA) unaotekelezwa na Mkandarasi Dyname Construction Engineering, na mitaa 10 iliyobaki itafikishiwa umeme katika miradi inayofuata.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Wanawake (UWT), Mhe. Zaytuni Swai aliyeuliza kuhusu jinsi Serikali ilivyojipanga kupeleka umeme maeneo ya pembezoni mwa mji wa Arusha hususan kwenye Kata ya Telat, Mhe. Kapinga ameeleza kuwa, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali katika maeneo ya pembezoni (Peri Urban) kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambayo lengo lake ni kusambaza umeme maeneo ya pembezoni mwa mji.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Cecilia Pareso alyeuliza kuhusu Vitongoji vya Wilaya ya Karatu kutokuwa na umeme na vichache vilivyo kwenye mradi kupelekewa nguzo 40 ambazo hazitoshelezi mahutaji na kuiomba Serikali kuongeza idadi hiyo, Mhe. Kapinga amesema kuwa kwa kawaida miradi ya Vitongoji inawigo kulingana na kazi aliyopewa Mkandarasi, hata hivyo amesema kuwa Wilaya ya Karatu ipo katika mradi wa Vitongoji 9,000 ambao utaanza kutekelezwa hivi karibuni na kusisitiza kuwa, miradi ya kupeleka umeme kwenye Vitongoji ni endelevu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...