Mwandishi Wetu,Dodoma.
BENKI ya NMB na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) wametiliana saini Mkataba wa makubaliano (MoU) juu ya ushirikiano katika kukuza uwezo wa kiteknolojia na Tehama kwa lengo la kushirikiana katika kukuza bunifu.
Mkataba huo unalenga kukuza uwezo wa Watanzania katika masuala ya kitehama lakini pia kuendelea kuchochea mabadiliko makubwa ya kidigitali yanayohusiana na sekta ya fedha.
Afisa Mkuu Rasilimali watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay ameongoza timu ya wataalamu wa Benki hiyo katika kutiliana saini huku Chuo kikuu cha Dodoma kikiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Profesa Lughano Kusiluka.
Akizungumza kuhusu mpango huo, Akonaay amesema katika makubaliano hayo wanalenga kuibua na kuendeleza vipaji mbalimbali ili kubaini wanafunzi wanaofanya vyema zaidi katika fani ya Tehama (ICT).
Amesema NMB itawapatia ushauri na kuwakuza kiuwezo, kuwapatia nafasi ya mafunzo kwa vitendo na kuwapa fursa ya kutekeleza mawazo walionayo, lakini kutoa mafunzo kwa kampuni changa kupitia programu za kuongeza ujuzi yaani (accelerator program).
Akonaay amesema kupitia mpango huo, wanafunzi wa UDOM watapata jukwaa maalum la kufanya majaribio ya bunifu za kiteknolojia zitakazokuwa na mrengo wa masuala ya kifedha na kuwapa fursa za kuendelea kubuni teknolojia katika sekta ya fedha (kwa mfumo wa NMB Sandbox).
Amesema hadi sasa kuna wabunifu zaidi ya 300 ambao wamejisajili katika mfumo wa sandbox wanaofanya tafiti za bunifu zao ikiwemo wanafunzi na kampuni changa za tehama yaani startups ambazo wanategemea kuziunga kwenye mfumo wa kibenki.
“Kwa kufanya hivi, Benki ya NMB inalenga kuhimiza na kukuza tamaduni ya kuja na teknolojia zinazohamasisha ujasiriamali lakini pia utatuzi wa changamoto mbalimbali katika sekta hii ya fedha,” amesema.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Benki ya NMB inaamini katika mabadiliko ya kidigitali ndiyo maana wamewekeza huko hivyo matamanio yao ni kuona wanafunzi kutoka UDOM wakiwa mstari wa mbele katika safari ya mabadiliko ya kidigitali.
Kwa upande wa elimu ya Fedha amesema NMB inatambua umuhimu wake elimu ya fedha kwa vijana wetu, tutaendelea kutoa elimu ya fedha ili kuweza kuwafanya wanafunzi, walezi na wazazi kuwa na uelewa kuhusu masuala ya kifedha na kuweza kufanya maamuzi sahihi ya fedha kila wakati na hii itasaidia katika nyanja mbalimbali za kimaisha kwani ni muhimu kufahamu vitu kama Bajeti na uwekezaji ulio bora wa fedha zako.
Kwa upande mwingine amesema makubaliano hayo yanahitaji ushiriki kwa pande zote kuanzia wanafunzi, uongozi wa Chuo na Benki ya NMB jambo linaloweza kukuza teknolojia hapa nchini na Afrika kwa ujumla.
NMB katika mpango wake wa NMB Foundation, wamesema wanaendelea kutoa ufadhili kwa wanafunzi yaani ‘Scholarships’ kupitia programu ya ‘Nuru Yangu’ ambapo wametumia zaidi ya Sh1 bilioni kuwezesha wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu kusoma kwenye vyuo vikuu vya serikali kikiwemo Chuo kikuu cha Dar es Salaam mwaka jana ambapo pamoja na ada, wanafunzi wanapewa, vifaa vya Chuo, nauli, bima ya afya na komputa mpakato na kwa UDOM wapo wanafunzi 50.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Udom Profesa Lugano Kusiluka amesema mpango huo unakwenda kuwakomboa na kufanya malengo yao katika Tehama yaweze kufahamika.
Profesa Kusiluka amesema Mkataba baina yao na NMB waliungoja kwa hamu kubwa kwani malengo yao ni kuzalisha waataalamu wenye ujuzi ndani na nje ya Afrika ili waweze kuvutia watu wengi zaidi waende Udom kujifunza.
Rais wa Serikali ya wanafunzi wa Udom Mohamed Abdallah Mohamed amesema mpango huo ndiyo mkombozi kwao na hivyo wanajiandaa kuwa wabobezi na mabilionea ambao wanalenga kujiajiri.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...