Na Mwandishi Wetu
MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, kutokea Mkoa wa Morogoro Dkt. Ally Simba, ametetea vikali hatua ya Tanzania kuwakatalia kuingia nchini baadhi ya raia wa kigeni na kuwakamata wengine, akiwemo mwanaharakati Boniface Mwangi, akisisitiza kuwa hatua hiyo ilikuwa halali na ya kulinda uhuru wa taifa.
Akiandika kutoka Nairobi nchini Kenya, ambako yuko katika ziara ya kikazi, Dkt. Simba ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Shirika la Mawasiliano Afrika Mashariki (EACO) lenye makao yake makuu Kigali, Rwanda, amesema watu hao hawakuja kwa nyadhifa za Serikali ya Kenya bali walikuja kwa nafasi zao binafsi, hivyo si sahihi kudai kuwa kuzuiwa kwao kunaleta mgogoro wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Kenya.
Amesema amekuwa akifuatilia kwa karibu mijadala inayoendelea katika vyombo vya habari vya kawaida na mitandaoni nchini Kenya, ambapo baadhi ya watu wameunga mkono hatua ya Tanzania huku wengine wakionesha mashaka au upinzani.
Hata hivyo, Dkt. Simba amesema hayo ni majadiliano ya kidemokrasia yanayopaswa kuenziwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini ukweli unabaki kuwa Tanzania haijakiuka sheria yoyote ya kimataifa wala kuhatarisha uhusiano wa kidiplomasia.
Kwa mujibu wa Dkt. Simba, hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Tanzania ilikuwa ya kulinda utaratibu wa kisheria wa ndani ya nchi, hasa ikizingatiwa kwamba raia hao wa kigeni walikuwa wakilenga kushiriki au kuathiri kesi nyeti inayomkabili kiongozi wa upinzani, Tundu Lissu, ambaye anakabiliwa na mashitaka ya uhaini.
Ametahadharisha kuwa hatua hiyo haipaswi kuchukuliwa kama njama ya kuzuia upinzani bali ni namna ya kulinda taasisi za kisheria na uhuru wa taifa.
Amesisitiza kuwa nchi yoyote inayojali utawala wa sheria haipaswi kuruhusu wageni kuingia na kujaribu kuathiri kesi za ndani, bila kujali misimamo yao ya kisiasa. Kwa mujibu wake, Boniface Mwangi anaripotiwa kuingia nchini kwa kutumia taarifa zisizo sahihi, jambo ambalo ni kosa katika sheria yoyote ya uhamiaji duniani. Wengine walijaribu kuvuka mipaka bila kutoa maelezo sahihi ya malengo ya safari zao—jambo ambalo si dogo.
Ameongeza kuwa, kwa uzoefu wake wa kusafiri mara nyingi katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini na Kongo, hajawahi kukumbana na matatizo yoyote kwa sababu huwa anaheshimu sheria za nchi husika, akihakikisha kuwa nyaraka zake ziko sahihi na sababu za safari zimeelezwa wazi.
Dkt. Simba amesema uhuru wa kujieleza haumaanishi uhuru wa kukiuka sheria za nchi nyingine, na mshikamano wa Afrika Mashariki haupaswi kuchanganywa na vitendo vya ukaidi dhidi ya taratibu za ndani za taifa huru.
Amepongeza uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa busara aliyoionesha katika kushughulikia tukio hilo, akisema Rais amedhihirisha kuwa Tanzania inathamini haki za binadamu, ushirikiano wa kikanda, lakini pia haitavumilia mtu yeyote kujaribu kuivuruga.
Aidha, amesisitiza kuwa uhusiano wa Tanzania na Kenya ni wa kindugu unaotegemea heshima ya pande zote mbili na si vitendo vya wachache wanaojaribu kuingiza siasa katika mchakato wa sheria.
Amesema nchi nyingi duniani kama Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimewahi kuchukua hatua kama hizo kwa raia wa kigeni waliotishia usalama au kujaribu kuathiri utaratibu wa kisheria, hivyo hatua ya Tanzania si ya kipekee wala ya kushangaza.
Kwa kumalizia, Dkt. Simba amepongeza uongozi wa Rais Dkt Samia kwa kusimama imara katika kulinda heshima na uhuru wa taifa, akisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya kulinda misingi ya sheria, amani na utulivu wa nchi. Amesema Tanzania imeonesha mfano wa uongozi unaojali nchi na si umaarufu wa muda mfupi, na kwamba yeye binafsi anajivunia kuwa Mtanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia.
Imeandikwa kwa muhtasari wa makala ya Dkt. Ally Yahaya Simba, Katibu Mtendaji wa EACO na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kutoka Morogoro Mjini, akiwa Nairobi, Kenya.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...