Na Diana Byera – Bukoba


Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, amezindua rasmi huduma za madaktari bingwa mkoani humo na kuwahimiza wananchi kuachana na imani za kishirikina kwa kuhusisha maradhi na uchawi, badala yake watumie huduma za kitabibu zilizopo ili kuboresha afya zao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Bi. Mwassa alisema jumla ya madaktari bingwa 41 wanatarajiwa kutoa huduma kwa muda wa siku tano, kuanzia Mei 5 hadi Mei 9, 2025.

"Umezuka mtindo wa watu kusingiziana uchawi—anayeumwa amelogwa, anayekufa kuna mkono wa mtu. Watu wamesahau kwenda hospitali kupata matibabu. Haujalogwa, njoo utibiwe tatizo lako kwa sababu huduma za magonjwa yote ya kibingwa zimetufikia karibu," alisema Mwassa.

Ameeleza kuwa serikali inaendelea kuimarisha huduma za afya katika mikoa ya pembezoni, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kisasa pamoja na dawa za kutibu magonjwa mbalimbali. Alisisitiza kuwa huduma hizi za kibingwa zinazotolewa na timu ya “Madaktari Bingwa wa Samia” pia zinaimarisha utalii wa matibabu, na zinatarajiwa kuvutia wagonjwa kutoka nchi jirani.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Dkt. Mseleta Nyakiroto, alisema kuwa tayari watu 2,000 wamejitokeza katika siku ya kwanza ya zoezi hilo, na idadi hiyo imevuka matarajio ya awali ya kuwahudumia wananchi 1,500.

“Tunaamini kuwa uwepo wa madaktari bingwa utasaidia kutoa mafunzo kwa madaktari wa ndani, na pia kupunguza rufaa nyingi ambazo wananchi walikuwa wakipewa kwenda hospitali za kanda au taifa,” alisema Nyakiroto.

Naye Mwenyekiti wa Waganga Wafawidhi wa hospitali za Kanda ya Ziwa, Kibwana Mfaume, alisema kuwa kaulimbiu ya timu hiyo ni: “Madaktari Bingwa wa Samia tumekufikia ulipo, karibu tukuhudumie.” Aliongeza kuwa kuanzia Mei 12, 2025, halmashauri zote za mkoa wa Kagera zitapokea madaktari bingwa katika hospitali za wilaya.

Alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata matibabu, akisisitiza kuwa serikali inatambua gharama na changamoto zinazowakumba wananchi kusafiri kwenda mbali kutafuta huduma hizo.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...