Na Mwandishi wetu 


WANAFUNZI  wenye vipaji katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano kutoka vyuo vikuu 12 duniani, wameshiriki katika kambi ya mafunzo ya kimataifa ya Huawei Global Seeds for the Future, iliyofanyika kuanzia Aprili 9 hadi Aprili 17, 2025 katika makao makuu ya Huawei huko Shenzhen nchini China. 

Kambi hiyo ya mafunzo ilibeba maudhui yenye lengo la kuwaongezea uwezo wanafunzi hao katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na eneo la kidigiti, ubunifu na ujasiriamali. 

Kambi hiyo iliyodumu kwa muda wa wiki moja ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo ya teknolojia ya mawasiliano ya Huawei katika kuendelea kuwawezesha vijana wenye vipaji katika sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano. 

Nchi zilizoshiriki kambi hiyo ya mafunzo nchini China ni pamoja na Tanzania, Algeria, Cambodia, Laos, Uturuki, Ireland, Brazil, Mexico, Azerbaijan, Pakistan, Ethiopia na Afrika Kusini. 

Akizungumzia mkakati huo wa Huawei, mmoja wa wanufaika kutoka  Tanzania akiiwakilisha Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa nne wa Shahada ya kwanza ya Sayansi katika Uhandisi wa Kielektroniki na Mawasiliano, Natasha Nassoro amesema mada za mwaka  huu hazikuacha mshiriki  yeyote nyuma akiweka bayana kuwa walijifunza mambo ya ndani na nje ya tasnia ya Tehama (ICT ) chini ya mpango ulioandaliwa vyema, ukihusisha utafiti na kupendekeza teknolojia tofauti za kuchagiza juhudi za uendelevu duniani chini ya mpango wa tech4good pamoja na kujenga na kuunganishwa na mtandao wa mabingwa wengine wenye vipaji. 

Ujumbe wa wanafunzi hao kutoka vyuo 12 duniani pia ulipata fursa ya kufanya ziara katika vituo vya maendeleo ya kiteknolojia kama vile kampuni  ya Alibaba, kituo cha mafunzo cha Huawei Global, Red note, duka la Huawei Flagship pamoja na  ziara za kitamaduni huko Shanghai, kutembelea mgahawa maarufu duniani na ziara ya ya kutembelea Jiji la Shenzhen.

 Huawei ilizindua programu ya Seeds For the Future nchini Thailand mwaka 2008, na hadi kufikia mwaka huu imefanikiwa kuwakusanya pamoja wanafunzi kutoka nchi 141 duniani huku zaidi ya wanafunzi 18,000 wakinufaika. 

Seeds for the Future ni programu kuu ya Huawei ya kurudisha kwa jamii (CSR), na imekuwa ikiendeshwa kwa kuchagua vipaji vya vijana kutoka duniani kote ili kushiriki katika mafunzo ya muda mfupi yanayolenga kuwashindanisha kwenye teknolojia, kubadilishana tamaduni na kukuza moyo wa ujasiriamali. 

Mpango huo umekuwa pia ukitoa nafasi ya upendeleo kwa wanawake kwa kiwango cha ushiriki cha angalau theluthi moja wawe wanafunzi wa kike.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...