Na. Brigitha Kimario- Serengeti
HIFADHI ya Taifa ya Serengeti ambayo ni miongoni mwa Hifadhi zenye hadhi ya urithi wa Dunia tangu mwaka 1981 inatarajia kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Urithi wa Dunia yanayotarajiwa kufanyika Mei 05, mwaka huu katika mji wa Mugumu wilayani Serengeti. Lengo likiwa ni kutoa elimu ya umuhimu wa kuyatunza maeneo haya na kuendeleza ushirikiano na wananchi katika ulinzi wa Hifadhi za Taifa zilizopo nchini.

Maadhimisho hayo yatahusisha kuonyesha maonesho mbalimbali ya vivutio vilivyopo katika vituo vya urithi wa Dunia na Taifa kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi hali itakayosaidia kuongeza uelewa na kuzifahamu sheria za Uhifadhi hususani kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya pembezoni mwa hifadhi.

Akizungumzia Maadhimisho hayo, eneo la Seronera Hifadhini Serengeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa uhifadhi, Stephano Msumi ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti alieleza maadhimisho haya yamekutanisha viongozi wa vituo vya urithi wa Dunia na Taifa kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambayo ni maeneo saba yalitambuliwa kuwa maeneo ya urithi kwenye kikao cha 38 cha kamati ya Shirika la Umoja wa mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mwaka 2015.

"Vituo vilivyotambuliwa ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa Mlima Kilimanjaro, maeneo ya michoro ya Mwambani Kondoa, Pori la akiba Selous, Magofu ya Kilwa Kisiwani, Songo Mnara na Mji mkongwe wa Zanzibar tunawakaribisha wananchi wa mkoa wa Mara kujitokeza kupata elimu juu ya maeneo haya muhimu”. amesema Msumi.

Kamishna Msumi alisema kuwa tukio la Maadhimisho ya Urithi wa Dunia na Afrika yatakayofanyika Mugumu, Mgeni Rasmi atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi ambaye atashiriki maandamano na kufunga kesho hafla ya Maadhimisho hayo ya siku ya Urithi Duniani.

"Ikumbukwe kuwa maadhimisho hayo yataanza majira ya asubuhi kwa maandamano ya matembezi ya umbali wa kilomita nne ambayo yataongozwa na Mkuu wa mkoa huyo,"amesema.

Zuberi Mabie ni Mhifadhi kutoka Kituo cha Kondoa Irangi anasema lengo hasa la maadhimisho hayo ni kuufanya umma uweze kutambua umuhimu wa maeneo yote yenye urithi wa dunia uliyopo nchini Tanzania .

"Maadhimisho haya yanalenga kuwafikia wananchi kwa kutambua baadhi ya maeneo hayo na kupata taarifa za kutosha kuhusu vituo vya urithi wa dunia na tutatoa fursa ya wao kufahamu umuhimu wake ili na wao wajione ni sehemu ya urithi huo wakishiriki kutatunza kwa kizazi cha sasa na kijacho” amesema Mhifadhi Mabie.

Nao baadhi ya Viongozi wa vituo hivyo wanabainisha changamoto wanazokutana nazo katika ulinzi wa maeneo hayo ni kuathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi, uvamizi wa maeneo ya hifadhi hali inayopelekea migogoro ya binadamu na wanyama pamoja na mioto.

Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo mwaka huu ni “Majanga na uharibifu ni kichocheo kikubwa kwenye maeneo ya hifadhi”.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...