Chama Kikuu cha Ushirika cha mkoa wa Shinyanga (SHIRECU LTD) kimekanusha vikali madai yanayoilamikia Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kumtuhuhumu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe kupora na kujimilikisha mali za Ushirika ambayo ni maghala ya Chama hicho yenye thamani ya milioni 900.
Madai hayo yamekanushwa na Mwenyekiti wa Bodi wa Chama hicho Lenis Izengo katika kikao na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na wajumbe wa Bodi wa Chama hicho kilichofanyika Jijini Dodoma.
" Sisi SHIRECU tumesikitishwa sana na taarifa hizi zilizosambazwa kwenye Vyombo vya Habari ikiwemo Youtube Channel ya "MW"na gazeti la Jamhuri, tunapinga vikali madai haya, kama Chama tunasimamia Chama kwa kufuata Sheria, taratibu, kanuni na miongozo ya Vyama vya Ushirika, hakuna mali yoyote ya SHIRECU iliyoporwa na Serikali kupitia Waziri wa Kilimo.
Ameongeza kuwa Serikali inafanya jitihada kubwa sana kuvisaidia Vyama vya Ushirika kwa kugawa pembejeo za Kilimo kwa Wakulima na kuhakikisha kuwa Vyama vya Ushirika vinaweza kusimama na kujiendesha kiuchumi, kwahiyo sio rahisi kuingilia mali za Chama ambazo ziko chini yake.
Katika kikao hicho, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege amekitaka Chama hicho kusimama kwenye nafasi yake na kusimamia, kutetea na kufanya shughuli zake pasipo kuingiliwa na mtu yeyote kwa maslahi mapana ya Chama hicho.
" Msiruhusu mtu yeyote asiye mwanachama kuzungumzia Chama chenu kwa maslahi yake binafsi, anzeni kutangaza mazuri yanayofanywa na Chama chenu kupitia Vyombo vya Habari ili jamii ione mafanikio zaidi kuliko changamoto" amesema Mrajis
Aidha, amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika kama msimamizi wa Vyama vya Ushirika itaendelea kuisaidia SHIRECU katika kuendeleza mipango na mikakati iliyonayo ya kimaendeleo inayofanywa kuendeleza Chama hicho.
" Niwahakikishie kuwa nitakuwa na nyie katika hatua zote za kimaendeleo, lakini nanyi msimame kwenye nafasi yenu msiruhisu mtu yeyote kukichafua Chama chenu kwa maslahi yake binafsi"
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Viongozi wa TCDC na Wajumbe wa Bodi ya SHIRECU.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...