Na Jane Edward, Arusha
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yamefanyika kwa hamasa kubwa katika jiji la Arusha huku serikali ikiahidi kushughulikia kwa vitendo changamoto zote zilizowasilishwa na wafanyakazi kupitia vyama vyao.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Joseph Mkude, aliwahakikishia wafanyakazi kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu na yenye nia ya dhati ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi nchini.
“Serikali ya Mama Samia imedhamiria kuona maisha ya wafanyakazi yanaboreshwa kwa kuzingatia haki zao za msingi, mazingira bora ya kazi na ushirikishwaji katika maamuzi yanayowahusu,” alisema Mhe. Mkude.
Katika upande mwingine, Kituo cha utafiti wa kilimo (TARI) Seliani, kupitia kwa Mkurugenzi wake Dkt. Karesma Joseph Chuwa, ilisisitiza dhamira yake ya kushirikiana kwa karibu na wafanyakazi wake ili kujenga mshikamano na ufanisi mahali pa kazi.
Dkt. Chuwa alieleza kuwa taasisi hiyo inaendelea kuwekeza katika tafiti za kilimo zenye tija, huku ikijikita kwenye ukuzaji wa mbegu bora zinazohimili mabadiliko ya tabianchi, hususan kwa mazao ya bustani (hot culture crops).
“Tumejipanga kuhakikisha tafiti zetu zinakuwa suluhisho la changamoto za kilimo, tukianzia na kuwahusisha wafanyakazi wetu kikamilifu katika mchakato mzima wa utafiti hadi utekelezaji,” aliongeza Dkt. Chuwa.
Maadhimisho haya yamebeba ujumbe mzito wa mshikamano, uwajibikaji na matumaini mapya kwa wafanyakazi kote nchini, huku yakisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, waajiri na wafanyakazi katika kuijenga Tanzania mpya yenye maendeleo jumuishi.
Aidha, Dkt. Chuwa alibainisha kuwa TARI Selian imeweka mkakati maalum wa kushughulikia changamoto ya utapiamlo kwa kufanya tafiti na kuzalisha mbegu bora zenye virutubisho vya kutosha ili kuhakikisha jamii, hususani watoto na wanawake wajawazito, wanapata lishe bora.
Alisema taasisi hiyo inatambua mchango wa kilimo katika afya ya jamii na hivyo haitajikita tu kwenye uzalishaji bali pia katika kuhakikisha usalama wa chakula na lishe.
Kwa mujibu wa Dkt. Chuwa, TARI Selian kwa sasa inahudumia Kanda ya Kaskazini kwa weledi wa hali ya juu, huku pia ikifanikiwa kuwafikia zaidi ya wakulima milioni mbili nchini kote kupitia mafunzo, tafiti na huduma za kitaalamu za ugani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...