• Benki ya Stanbic Tanzania yazindua kampeni mpya ya Salary Switch, inayotoa zawadi za kila siku za pesa taslimu na mikopo ya mshahara kwa wafanyakazi waliopata ajira rasmi.
• Kampeni inalenga kuimarisha uthabiti wa kifedha wa muda mrefu kwa kuhamasisha kuweka akiba kwenye akaunti za watoto, na kukuza utamaduni wa kuokoa.
• Droo za bahati nasibu zinatoa fursa kwa wafanyakazi kote Tanzania kujishindia zawadi kubwa za pesa kwa urahisi kwa kutumia huduma za Stanbic Bank.
Dar es Salaam, Tanzania – Jumatatu, 17 Machi 2025 – Benki ya Stanbic Tanzania leo imezindua rasmi kampeni mpya ya Salary Switch, inayolenga kuwazawadia Watanzania waliopo kwenye ajira rasmi kwa zawadi za kila siku za pesa taslimu, mikopo ya mshahara ya kidigitali, na upatikanaji rahisi wa mikopo hadi TZS milioni 150. Kampeni hiyo ya miezi mitatu itaanza tarehe 1 Mei hadi 30 Julai 2025, na inalenga wafanyakazi wa sekta binafsi na ya umma, kuwapatia urahisi wa kifedha wa haraka, motisha, na huduma bora za kidigitali.
Kupitia kampeni hii, wateja watakaohamishia mishahara yao Stanbic Bank wataweza kushiriki kwenye droo za bahati nasibu za kila siku (Jumatatu hadi Ijumaa), zenye zawadi za pesa taslimu zinazotofautiana kati ya TZS 100,000 hadi TZS 500,000 kulingana na siku.
Zaidi ya hayo, wateja wanaofungua Akaunti ya Akiba ya Mtoto (Hatua) watazawadiwa na benki kwa kulinganisha kiasi cha awali kilichowekwa hadi TZS 250,000, ili kuwapa watoto wao mwanzo mzuri wa kifedha. Kwa wateja waliofungua akaunti hiyo tayari, kuweka amri ya kudumu ya kujiwekea akiba pia kutaleta zawadi kama hiyo – benki italinganisha kiasi kinachowekwa hadi TZS 250,000.
Akizungumza wakati wa uzinduzi uliofanyika makao makuu ya Stanbic Bank jijini Dar es Salaam, Emmanuel Mahondaga, Mkuu wa Kitengo cha Wateja binafsi na mauzo, alisema kuwa kampeni hii inaonesha dhamira ya benki ya kuboresha huduma kwa wateja kwa suluhisho za kifedha bunifu.
“Tunatambua kuwa wafanyakazi na familia zao ni sehemu muhimu ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania. Kupitia zawadi za pesa kila siku, mikopo ya mshahara ya papo kwa papo hadi 60% ya mishahara yao, na fursa za mikopo hadi TZS milioni 150, tunahakikisha wateja wetu wanapata huduma za kifedha zinazowasaidia katika maisha yao ya kila siku,” alisema Mahondaga.
Priscus Kavishe, Meneja Mwandamizi wa Mauzo, alisisitiza umuhimu wa kuhamasisha utulivu wa kifedha na uwekaji wa akiba kwa muda mrefu kupitia akaunti ya mtoto ya Hatua.
“Kupitia akaunti ya Hatua, tunawahamasisha wazazi kuwekeza kwa ajili ya mustakabali wa kifedha wa watoto wao. Tutaendelea kulinganisha amri za kudumu hadi TZS 250,000 kwa mwezi wakati wa kampeni hii. Hii ni zaidi ya zawadi – ni kuhusu kuwasaidia familia kujijengea uthabiti wa kifedha wa baadaye,” alisema Kavishe.
Kwa uwazi na usawa, kila mteja atakayefanikisha kuanzisha akaunti ya mshahara ya “Wezesha” atapokea ujumbe mfupi (SMS) kuthibitisha ushiriki wake katika droo ya kila siku. Washindi watatangazwa kila siku kuanzia mwezi wa pili wa kampeni. Mchakato huu ni wazi na umeundwa ili kuwazawadia na kuwaunga mkono wateja wanaoichagua Stanbic kama mshirika wao wa kifedha.
Wateja wanaotaka kushiriki wanaweza kufungua akaunti zao katika matawi yote ya Stanbic Bank au kwa kutumia programu ya simu ya Stanbic au tovuti ya benki kwa urahisi na usalama wa kidigitali. Stanbic pia inashirikiana na waajiri kuhakikisha mishahara ya wafanyakazi inahamishiwa moja kwa moja kwenye akaunti zao mpya.
Stanbic Bank Tanzania, sehemu ya Standard Bank Group – taasisi kubwa zaidi ya huduma za kifedha barani Afrika – inaendelea kutumia ubunifu kuwakwamua Watanzania na kuhakikisha huduma za kibenki zinapatikana kwa urahisi, usalama, na kwa manufaa zaidi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...