Baadhi ya wanachama wa TPDC Runners Club wakiwa katika picha ya pamoja

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) leo limeungana na wadau mbalimbali katika kushiriki mbio za marathoni zilizoandaliwa kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini. Mbio hizo zimefanyika katika viwanja vya Green Ground, Oysterbay jijini Dar es Salaam na zimehusisha wakimbiaji katika kategoria mbalimbali za umbali wa kilomita 5, kilomita 10 na kilomita 21.

TPDC, kama taasisi ya umma yenye jukumu la kusimamia maendeleo ya rasilimali za mafuta na gesi asilia nchini, imeona umuhimu wa kutumia jukwaa hili kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu faida za kutumia nishati safi ya kupikia, hususan gesi asilia majumbani, kwa afya ya jamii na mazingira.

Katika kuhakikisha mafanikio ya tukio hili muhimu, TPDC imetoa udhamini wa shilingi milioni 20, ikiwa ni mchango wake katika kufanikisha maandalizi na uendeshaji wa mbio hizo. Udhamini huu ni sehemu ya dhamira ya Shirika katika kushirikiana na jamii kwenye shughuli za michezo.

Akizungumza kwa niaba ya TPDC, Mkurugenzi wa Biashara ya Gesi na Mafuta Mha.Emmanuel Gilbert alisema

"Ushiriki wetu katika mbio hizi ni sehemu ya jitihada za shirika kuendelea kuhamasisha matumizi ya gesi asilia kama nishati safi ya kupikia, ambayo ni salama, rafiki kwa mazingira na yenye gharama nafuu kwa wananchi."

Mbali na kutoa udhamini, TPDC imeshiriki kikamilifu katika mbio hizo kupitia wanachama wa klabu yake ya ‘TPDC Runners’. Klabu hii imekuwa ikishiriki matukio mbalimbali ya michezo nchini kwa lengo la kulitangaza Shirika, kuimarisha afya za wafanyakazi, pamoja na kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia. Wanariadha wa TPDC Runners wameonesha ushindani na ari kubwa ya kushiriki, wakibeba ujumbe maalum juu ya umuhimu wa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa, na badala yake kuchagua gesi asilia kama mbadala salama, nafuu na rafiki wa mazingira.

Frank Maziku -Mkimbiaji kutoka TPDC Runners Club

Kupitia ushiriki huu, TPDC inazidi kudhihirisha dhamira yake ya kuchangia katika ajenda ya taifa ya upatikanaji wa Nishati Safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya madhara ya kiafya na kimazingira yatokanayo na matumizi ya nishati chafu ya kupikia.

Katika hatua nyingine baadhi ya wanariadha kutoka TPDC walitoa maoni yao kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi:

“Mimi ni mtumiaji wa gesi asilia nyumbani. Ni salama kwa familia yangu na imenipunguzia gharama kubwa za kuni na mkaa,” alisema Bi. Eva Swilla wa TPDC Runners Club.

“Mbio hizi zimeleta uelewa kwa jamii. Tunaamini tukirudia mara kwa mara, tutaweza kubadilisha fikra za wengi kuhusu kupika kwa kutumia Nishati safi,” aliongeza Bi.Delian Kabwogi, mwanariadha kutoka TPDC.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...