SONGEA-RUVUMA.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Mkoa wa Ruvuma, Wakili Eliseus Ndunguru, amesema kuwa wananchi wana haki ya kutoa maoni yao, lakini uhuru huo unapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia sheria na kuheshimu haki za watu wengine, ili kuimarisha mshikamano na amani katika jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea Ndunguru amesema uhuru wa kutoa maoni ni mojawapo ya haki za msingi zilizoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini si ruhusa ya kuvuruga utaratibu wa kisheria au kuhatarisha usalama wa wengine.

Wakili huyo ameeleza kuwa moja ya changamoto kubwa katika jamii ya Watanzania ni uelewa mdogo kuhusu mipaka ya haki za kikatiba kama vile uhuru wa maoni, amesema hali hiyo imechangia baadhi ya watu kujikuta katika matatizo ya kisheria kwa kutoa kauli au maandiko yenye madhara kwa jamii bila kujua kuwa wanakiuka sheria.

Amebainisha kuwa mitandao ya kijamii imekuwa jukwaa kubwa la maoni, lakini matumizi yake yamechochea migongano mingi kutokana na ukosefu wa maadili na nidhamu ya matumizi ya lugha, amesisitiza kuwa ni muhimu wananchi watambue kuwa uhuru huo ni wa kisheria na si wa kiholela.

“Sheria zipo na zinaelekeza namna ya kutumia uhuru huu. Hatutaki kuzuia watu kusema, bali tunataka wahakikishe kuwa wanazingatia mipaka ya kisheria ili kuzuia madhara kwa mtu binafsi na kwa jamii kwa ujumla,” aliongeza.

Ndunguru pia alisema kuwa elimu ya sheria ni jambo la msingi kwa kila mwananchi, na kwamba ni wajibu wa serikali, taasisi za kiraia na vyombo vya habari kuhakikisha kuwa elimu hiyo inawafikia watu wengi, hasa katika maeneo ya vijijini.

Aidha, amewahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika mijadala ya kisheria, kutoa maoni kwa njia ya staha na kutumia vyombo rasmi kutoa malalamiko badala ya kuchochea chuki au kujichukulia sheria mikononi.

Amesema licha ya sheria kuwa nzuri na za kutosha, lakini bado changamoto kubwa ipo kwa wale waliokabidhiwa kuzisimamia, ambapo baadhi yao hukosa utashi wa kutenda haki, Pia muingiliano wa kisiasa umekuwa kikwazo kwa weledi wa sheria katika kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Ndunguru ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa, kijamii na kidini kuwa mfano bora wa matumizi ya uhuru wa maoni, kwa kutoa kauli zenye kujenga jamii badala ya kuibomoa, ili taifa liendelee kuwa na mshikamano, haki na maendeleo endelevu.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...