Dar es Salaam, Mei 2025
WATAALAMU wa mawasiliano na usalama watumiaji wa mitandao ya simu wamewataka Watanzania kuwa makini zaidi kufuatia ongezeko la visa vya utapeli kupitia simu, huku wakisifu ubunifu wa kiteknolojia unaoongozwa na Airtel Tanzania, hususan huduma yao ya Airtel Spam Alert – Kataa Matapeli, kwa kusaidia wananchi kuwabaini matapeli mapema.
Akizungumza kuhusu hali ya sasa ya utapeli wa simu na umuhimu wa kujikinga kidijitali, Mary Shayo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC), alisema kuwa utapeli wa simu bado ni changamoto kubwa kwa watumiaji wa huduma hizo.
“Utapeli husababisha hasara kubwa ya kifedha na kupunguza imani ya wananchi katika mawasiliano ya simu. Lakini simu za mkononi ni sehemu muhimu ya maisha yetu ya kila siku – kiuchumi, kijamii na hata kikazi,” alisema Shayo.
Alisisitiza juu ya dhamira ya serikali kupambana na uhalifu wa kidijitali kupitia kampeni kama #SITAPELIKI, ambayo inalenga kuelimisha na kulinda watumiaji wa simu kote nchini. Aidha, alieleza kuwa ushirikiano na kampuni za mawasiliano na wabunifu wa teknolojia ni muhimu katika kuongeza uelewa na uwezo wa kupambana na matapeli.
“Tunawahimiza watumiaji wawe waangalifu kila wanapopokea ujumbe wa kutiliwa shaka. Kampeni yetu ya #SITAPELIKI, tunayoendesha kwa kushirikiana na mitandao yote ya simu, ni sehemu ya jitihada hizi. Katika hilo, tunaisifu Airtel Tanzania kwa ubunifu wake mkubwa wa Airtel Spam Alert – Kataa Matapeli, huduma inayotumia akili bandia (AI) kugundua ujumbe wa kitapeli kwa wakati halisi na kuwakinga wateja,” alisema.
Shayo aliongeza kuwa huduma hiyo inaonyesha dhamira ya Airtel kulinda watumiaji na inaendana na juhudi za kitaifa za kujenga mazingira salama ya kidijitali.
“Huu si ubunifu wa kiteknolojia tu, bali ni suluhisho halisi la kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi na kujilinda. Airtel wanastahili pongezi kwa kuonesha mfano na kuchukua jukumu,” alieleza.
Kwa upande wake, Florence Mtuka, mwakilishi kutoka Baraza la Ushauri kwa Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, alisema uwekezaji wa Airtel unaiunga mkono serikali katika lengo lake la kuhakikisha matumizi salama ya intaneti, hasa maeneo ya vijijini.
“Kadri mtandao unavyotanuka, tumeshuhudia ongezeko la matumizi ya simu, hata katika maeneo ya pembezoni. Watumiaji wengi wanabadilika kutoka simu za kawaida kwenda kwenye ‘smartphones’, jambo linalokuza fursa lakini pia hatari. Huduma kama Airtel Spam Alert, inayotumia AI kuchambua ujumbe kwa kuzingatia historia ya data, ni muhimu sana kwa wakati huu,” alisema Mtuka.
Alisisitiza kuwa ubunifu huu utasaidia sana serikali kulinda wananchi, hasa katika maeneo yenye uelewa mdogo wa uhalifu wa kidijitali.
“Haya ni mambo yatakayowezesha ukuaji wa huduma za kidijitali bila kuathiri usalama – jambo muhimu sana kwa maendeleo jumuishi ya kidijitali,” aliongeza.
Kwa niaba ya Airtel Tanzania, Beatrice Singano, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Kampuni, alieleza kuwa huduma ya Spam Alert inapatikana kote nchini na inaweza kutumika kwenye simu za kawaida na ‘smartphones’ pia.
“Mfumo huu wa AI huchambua na kubaini ujumbe unaotiliwa shaka na kuwaonya wateja mapema kabla ya madhara kutokea,” alisema Singano.
Aliwahimiza wateja kuchukua tahadhari binafsi kama kuhakikisha namba zao zimesajiliwa kwa majina yao sahihi, na kuendelea kuelimishana kwani matapeli hubadilika mbinu mara kwa mara.
“Tuendelee kuwa makini na kuelimishana. Airtel haitawahi kutuma ujumbe au kupiga simu kutoka namba yoyote zaidi ya 100. Huduma yetu mpya ya Airtel Spam Alert inawasaidia watumiaji kutambua kama ujumbe ni halali au wa kitapeli – hivyo kuwawezesha kufanya maamuzi salama,” alisisitiza. “Tunaungana na serikali kusema Kataa Matapeli. Kwa pamoja, tunaweza kuhakikisha teknolojia ya simu siyo tu inatuwezesha, bali pia inakuwa salama kwa kila Mtanzania,” alihitimisha Beatrice.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...