Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amefanya mkutano maalum na wamiliki pamoja na wahariri wa vyombo vya habari kwa lengo la kueleza mwelekeo mpya wa Wizara pamoja na matukio muhimu yatakayojiri katika mwezi Mei 2025.

Mkutano huo umefanyika jijini Dar es Salaam ambapo ajenda kuu ilikuwa ni uzinduzi wa Sera mpya ya Mambo ya Nje, sambamba na ratiba ya ziara za viongozi wa kimataifa zitakazofanyika nchini.

Akihutubia mkutano huo, Waziri Kombo amesema kuwa uzinduzi rasmi wa Sera mpya ya Mambo ya Nje utafanyika Mei 19, 2025. Amefafanua kuwa sera hiyo ni zao la maboresho ya Sera ya mwaka 2001, yaliyoanza kutekelezwa mwaka 2024, kwa lengo la kuiwezesha Tanzania kukabiliana na changamoto mpya za kisiasa, kiuchumi na kijamii katika mazingira ya ndani na ya kimataifa.

Waziri Kombo ameeleza kuwa vipaumbele vya sera hiyo ni pamoja na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika medani ya kimataifa kupitia diplomasia ya uchumi, kulinda maslahi ya taifa, na kukuza ushirikiano na mataifa pamoja na taasisi za kimataifa. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mazingira ya ndani yatakayowezesha utekelezaji mzuri wa sera hiyo.

Katika kuelekea utekelezaji wa sera hiyo, Waziri Kombo amesema kuwa Serikali imeandaa mikakati mahsusi, ikiwemo kushirikisha kikamilifu Watanzania waishio nje ya nchi (diaspora), kutumia Kiswahili kama bidhaa ya taifa, pamoja na kujumuisha masuala ya mazingira, usawa wa kijinsia na maendeleo ya vijana katika ajenda za kidiplomasia.

Mbali na uzinduzi wa sera hiyo, Waziri Kombo ametangaza kuwa Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa viongozi wa mataifa mbalimbali katika mwezi Mei. Amebainisha kuwa Rais wa Msumbiji, Mhe. Daniel Chapo, atafanya ziara ya kitaifa kuanzia Mei 7 hadi 9, Rais wa Finland, Mhe. Alexander Stubb, anatarajiwa kuzuru nchini kwa siku tatu kuanzia tarehe 16 hadi 19 Mei, huku Rais wa Namibia naye akitarajiwa kuwasili nchini Mei 21, 2025.













Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...