Na Nihifadhi Abdulla, Zanzibar
MKURUGENZI wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa, ametoa wito kwa waandishi wa habari nchini kuwa mstari wa mbele katika kuripoti vitendo vya udhalilishaji, matusi na vitisho wanavyokumbana navyo wanawake katika vipindi vya uchaguzi.
Akizungumza kwenye mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari katika ofisi za TAMWA Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja, Dkt. Mzuri amesema ukatili wa kisiasa dhidi ya wanawake ni changamoto inayodhoofisha ushiriki wao katika uongozi.
“Tumeona kwa miaka mingi wanawake wanaojitokeza kugombea au hata kushiriki kwenye kampeni hupigwa vita kwa lugha za matusi, kejeli, vitisho na hata shutuma zisizo na msingi. Sisi kama jamii, na ninyi waandishi, tunapaswa kusema hili halikubaliki lazima tumsaidie mwanamke asimame bila kuogopa,” amesema kwa msisitizo.
Dkt. Mzuri ameeleza kuwa waandishi wa habari wana nafasi ya kipekee ya kubadili mtazamo wa jamii kupitia kazi zao za habari zenye mwelekeo wa kijinsia na zinazojikita katika haki za binadamu zinaweza kubadilisha uelewa wa umma na kusaidia kuondoa vizingiti vinavyowakwamisha wanawake kwenye siasa. “Andikeni kwa ujasiri, simameni na ukweli, msiogope kusimulia kile kinachowapata wanawake wetu,” aliongeza.
Amesema kuwa TAMWA Zanzibar itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari ili kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa waandishi, hasa vijana, juu ya usawa wa kijinsia na mbinu bora za kuripoti ukatili wa kisiasa.
Ameongeza kuwa endapo waandishi watawezeshwa ipasavyo, wataweza kuwa chombo madhubuti cha mabadiliko ya kijamii na ya kisiasa hususan kwa kipindi hiki cha uchaguzi
Miongoni mwa waandishi walioudhuria mafunzo hayo Nusra Shaaban amesema mafunzo hayo yamewafumbua macho kuhusu namna ya kutambua ukatili wa kisiasa unaomkumba mwanamke na jinsi ya kuripoti kwa kuzingatia usalama wake. “Tulikuwa tunaona kama hawatendewi hakai wanawake lakini sasa tumemtambua kumbe ni ukatili unaofanyika waziwazi. Tumejifunza kua ngangari kuwatetea wanawake,”
Naye Ivan Mapunda, mwandishi wa habari kutoka Zenji Fm ameeleza kuwa kuna haja ya mashirika ya habari kushirikiana kwa karibu na mashirika ya kiraia kama TAMWA, ZAFELA PEGAO ili kuandaa vipindi vya redio na makala zinazomlinda mwanamke wakati wa uchaguzi. “Sisi waandishi tukiungana, tunaweza kuwafanya wanaodhulumu wanawake washindwe kimkakati” amesema
Waliomba vyombo vya habari kuweka sera za ndani zitakazolinda waandishi wa habari, hasa wanawake, wasikumbwe na hofu au mashinikizo wanaporipoti habari huku wakisisitiza kuwa ukimya wa vyombo vya habari unaleta nafasi kwa wahusika kuendeleza vitendo hivyo bila woga.
Jumla ya Waandishi wa habari 30 wa Unguja wamepatiwa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Dar es salaam UDSM yanalenga kuripoti na kukemea ukatili wanaofanyiwa wanawake kipindi cha Uchaguzi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...