Na Mwandishi Wetu,
Arusha, Tanzania – Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Profesa Eliamani Sedoyeka, amesema kuwa makubaliano ya ushirikiano (MOU) yaliyotiwa saini kati ya chuo hicho na Chuo Kikuu cha Heriot-Watt – Edinburgh cha nchini Uingereza kupitia shule yake ya biashara, ni hatua kubwa katika kukuza ubora wa elimu ya biashara nchini.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, Prof. Sedoyeka alisema ushirikiano huo utaimarisha mwelekeo wa kimataifa wa IAA kwa kutoa fursa zaidi kwa wanafunzi na wahadhiri kunufaika na maudhui ya kitaaluma ya kiwango cha juu duniani.

“Kupitia makubaliano haya, IAA sasa itakuwa na uwezo wa kutoa kozi za biashara zenye hadhi ya kimataifa, sambamba na kuanzisha kituo cha msaada wa kujifunza kwa wanafunzi wa Heriot-Watt hapa hapa Arusha,” alisema Prof. Sedoyeka.

Makubaliano hayo yana lengo la kufanikisha upatikanaji wa maudhui ya kitaaluma ya kimataifa kwa njia ya mtandao;Kuanzisha programu za kubadilishana wanafunzi na wahadhiri na kuwapa Watanzania na wanafunzi wa Afrika Mashariki fursa ya kusoma kozi za Heriot-Watt;

Mengine ni kuuwezesha msaada wa ana kwa ana kwa wanafunzi wanaosoma kupitia mtandao kwa kuanzisha kituo maalum ndani ya IAA.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Heriot Watt – Edinburgh Business School Profesa Angus Liang amesema ushirikiano huo ni sehemu ya mkakati wao wa kupanua wigo wa elimu ya ubora duniani kote, huku wakilenga maeneo yanayokuwa kwa kasi kama Afrika Mashariki.

Chuo Kikuu cha Heriot Watt ni miongoni mwa taasisi za juu duniani katika taaluma ya biashara, hasa kwa kutumia mbinu bunifu za kujifunza kwa njia ya mtandao. Ushirikiano huu unatarajiwa kuongeza mvuto wa IAA kwa wanafunzi wa ndani na nje ya nchi.

Tayari maandalizi yameanza ya kutekeleza vipengele vya makubaliano hayo, huku wanafunzi wa IAA wakitazamiwa kuanza kunufaika na baadhi ya kozi hizo ndani ya mwaka huu wa masomo.

“Ni wakati wa kujiandaa kimataifa, na kwa IAA tunasema: Elimu bora, fursa pana,” alihitimisha Profesa Sedoyeka.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...