Na Mwandishi Wetu, Mwananchi – Dodoma 4 Juni 2025

Katika banda hilo, lililo sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani yanayoendelea katika viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), wageni wamefurika kusikiliza maelezo kuhusu aina mbalimbali za mbegu za miti, uoteshaji bora na umuhimu wake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza na Mwananchi, Mhifadhi Emmanuel Christopher kutoka Kituo cha Uzalishaji wa Mbegu Bora za Miti – TFS Morogoro, alisema mbegu bora ni msingi wa misitu imara na endelevu, hasa kwa miti ya asili ambayo ina faida kubwa kiikolojia na kiuchumi lakini imeanza kupotea kwa kasi.
“Mbegu hizi tunazozalisha zimehakikiwa na zina kiwango cha juu cha uoteshaji. Lengo letu ni kuhakikisha wananchi na taasisi wanapata mbegu sahihi, wanapanda miti sahihi, na kwa njia sahihi, ili tufikie uhifadhi wa kweli,” alisema Christopher.
Aidha, alibainisha kuwa uhamasishaji kuhusu matumizi ya mbegu bora ni sehemu ya mkakati mpana wa kitaifa wa kuongeza upandaji wa miti, kupunguza uharibifu wa vyanzo vya maji, na kuendeleza matumizi ya nishati mbadala badala ya mkaa na kuni.
“Tunatoa mafunzo hapa kuhusu namna ya kuandaa vitalu, kuchagua aina ya mbegu kulingana na tabianchi ya eneo, na mbinu za kuongeza uoteshaji kwa kutumia teknolojia rahisi zinazopatikana kwa wakulima wa kawaida,” aliongeza.
Wakati huo huo, baadhi ya wananchi waliotembelea banda hilo walisema wamepata maarifa mapya kuhusu umuhimu wa kutumia mbegu sahihi na za asili, na kwamba wameamua kuanzisha vitalu katika maeneo yao kwa ajili ya upandaji wa miti ya kudumu.
“Kwa kweli nimejifunza mengi. Nilikuwa sijui kama kuna tofauti kubwa kati ya mbegu za kawaida na hizi bora. Nimechukua baadhi zenyewe hapa, nataka nipande nyumbani kwetu Chamwino,” alisema Neema Jumanne, mkazi wa Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...