Katika kuhakikisha elimu ya  nishati safi ya kupikia inamfikia kila Mtanzania, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange ametumia sehemu ya ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi ya umeme katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupika kwa umeme kwa viongozi wa  Serikali za Mikoa na Wilaya ili kuongeza uelewa zaidi kwa wananchi.

Bw. Twange ametumia nafasi hiyo  kuelimisha na kutoa zawadi za majiko janja yenye teknolojia inayotumia umeme kidogo kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Kenani Kihongosi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza  Mhe.Saidi Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi Pamoja na  Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Wakili Julius Mtatiro ikiwa ni sehemu ya Kampeni ya TANESCO ya kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia umeme.

Amesema  licha ya  Shirika hilo kujikitika katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme wa uhakika bado wanajukumu la kutekeleza kwa vitendo Ajenda  ya Mhe. Rais Dkt.  Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi kwa ajili ya kupikia na ametoa majiko hayo kwa viongozi wa Serikali ili kupata picha halisi ya unafuu wa kutumia umeme kupikia ili kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi.

‘’Vifaa hivi vinatumia umeme kidogo kwenye kupika na tumetoa majiko haya kwa ajili ya matumizi ya kupikia  ili mtusaidie kuwahamasisha na kuongeza uelewa kwa wananchi kwa kuwa mtakuwa mashahidi na  mabalozi wazuri wa kueleza faida za majiko hayo hatua itakayowavutia  zaidi wananchi kisha kubadili mitazamo’’ amesisitiza Bw Twange

Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Wakili Julius Mtatiro ameipongeza TANESCO kwa mkakati huo ambao unadhamira ya dhati ya kufanya mageuzi ya elimu ya matumizi ya nishati safi ili kuwafanya wananchi kuachana na matumizi ya nishati isiyo salama  zenye athari kiafya kwa watumiaji na chanzo cha uharibifu wa mazingira.

‘’Tumepokea zawadi ya jiko hili tunashukuru, tutaitumia mikutano yetu na wananchi kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi na wananchi wetu ni waaminifu ninaamini wataelewa na kwa sasa  tutawaelimisha kwa vitendo,’’ alifafanua Mhe. Mtatiro.

Ziara ya Mkurugenzi wa TANESCO Bw. Lazaro Twange katika Mikoa ya kanda ya ziwa imelenga kukagua miradi mbalimbali ya uzalishaji umeme lakini pia ametumia nafasi hiyo kuongeza msisitizo wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ya umeme ikiwa ni muendelezo wa kampeni inayofanywa na TANESCO ya kuhakikisha ajenda ya Serikali inafanikiwa.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...