Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
MKURUGENZI wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Rose Reuben, amesisitiza msimamo wa chama hicho katika kulinda heshima na utu wa mwanamke, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025. Ametoa wito kwa jamii na wanasiasa kujiepusha na siasa za matusi, kejeli na matamshi ya chuki yanayolenga kudhalilisha wanawake, hususan viongozi wa kisiasa.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa wanachama wa TAMWA unaofanyika jijini Dar es Salaam leo na kesho Juni 27, 28, 2025, Rose Reuben amesema mwaka huu wa uchaguzi, TAMWA itakuwa makini kufuatilia namna uchaguzi unavyoweza kutumika kama jukwaa la kudhalilisha wanawake kupitia lugha na vitendo visivyo vya kiungwana.

 “TAMWA itaangalia kwa karibu jinsi masuala ya uchaguzi yanavyoweza kutumika kutweza utu wa mwanamke. Hili hatutalikubali. Wanawake, hasa wanasiasa, wanapaswa kuheshimiwa kama binadamu na viongozi,” alisema Rose.

Ameeleza kuwa pamoja na teknolojia kuleta maendeleo chanya, changamoto kubwa imekuwa ni ukatili wa kijinsia unaofanywa kupitia mitandao ya kijamii, ambapo wanawake maarufu na viongozi wa kisiasa wamekuwa wahanga wa matusi, dhihaka na lugha za kuwadhalilisha.

 “Teknolojia inaleta mema, lakini imekuwa pia jukwaa la kudhalilisha wanawake. Inasikitisha sana kuona viongozi wanawake wakitukanwa, kudhalilishwa na kutishwa mitandaoni,” amesema kwa masikitiko.

Katika kuelekea uchaguzi, amewaomba Watanzania wote, bila kujali itikadi zao, kupingana kwa hoja na si kutumia lugha za chuki au kuwadhalilisha wengine.

 “Kiongozi wa kweli ni yule anayepingana kwa hoja, anayejua shida za Watanzania na anayetueleza atatufanyia nini. Sio kiongozi anayejitafutia umaarufu kwa kutukana au kutweza utu wa mwanamke,a huyo si mwanasiasa anayefaa,” amesisitiza.

Aidha, amesema kuwa matamshi ya chuki hayana nafasi katika mila na desturi za Kitanzania, ambazo zinahimiza heshima, utu na mshikamano.

Ameyataka vyama vya siasa na viongozi wao kuwekeza katika siasa safi za hoja na kujenga taifa lenye ustaarabu wa kisiasa na kijamii.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Mkurugenzi huyo alieleza fahari yake kwa kuwa na wanachama wa TAMWA kutoka vikao vyote vya umri, kuanzia wazee, watu wa makamo hadi vijana.

 “Hili ni jambo kubwa sana kwetu, kwani linatufanya tujifunze kwa njia mbili – wakubwa kujifunza kutoka kwa wadogo waliobobea katika teknolojia, na wadogo kujifunza busara na uzoefu wa wakubwa waliopita katika tasnia ya habari,” amesema Rose.

TAMWA inaendelea kuwa nguzo muhimu katika kulinda haki na ustawi wa wanawake nchini, hasa katika nyanja ya habari, uongozi na ushawishi wa kijamii.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...