Na Mwandishi Wetu – Dodoma 04 Juni 2025

Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis, leo ametembelea banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani yanayoendelea jijini Dodoma, na kuipongeza taasisi hiyo kwa kazi nzuri ya uhifadhi wa misitu na mchango wake katika maendeleo ya sekta mbalimbali.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo katika viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), Naibu Waziri alieleza kuridhishwa kwake na ubunifu na jitihada za TFS katika kulinda mazingira, akisema taasisi hiyo ni mfano wa kuigwa katika usimamizi wa rasilimali za misitu nchini.

“TFS mnafanya kazi kubwa ya kuendeleza na kuhifadhi misitu, lakini pia mnaushirikiano mzuri na sekta nyingine kama wanyamapori, kilimo, nishati na maji. Napongeza kazi yenu,” alisema Mhe. Khamis.

Katika maelekezo yake, Naibu Waziri alisisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi katika ukusanyaji, uhifadhi na usambazaji wa mbegu za miti ya asili ambazo zimeanza kupotea kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la shughuli za binadamu na ukosefu wa elimu kuhusu umuhimu wa miti hiyo.

“Mbegu za miti ya asili ni urithi wa Taifa, lakini nyingi zimeanza kutoweka. TFS mna jukumu muhimu la kuhakikisha zinapatikana na kuhifadhiwa kwa vizazi vijavyo,” alieleza.

Aidha, Mhe. Khamis alitoa wito kwa TFS kuongeza kasi ya kuhamasisha shughuli za ufugaji nyuki nchini, akibainisha kuwa ni sehemu ya uhifadhi endelevu na chanzo muhimu cha kipato kwa wananchi.

“Ufugaji wa nyuki si tu kwamba unalinda misitu, bali pia unaleta maendeleo ya kiuchumi kwa jamii. Tuwawezeshe wananchi walione hili kama fursa ya kweli,” aliongeza.

Awali, akimkaribisha Naibu Waziri, Mhifadhi Karimu Solyambingu wa TFS alieleza kuwa ushiriki wa wakala huyo katika maonesho hayo ni sehemu ya juhudi za kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa misitu na nyuki, na namna wananchi wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira.

Alisema TFS inatekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali na sekta binafsi, hasa katika maeneo ya hifadhi, uzalishaji wa miche, utunzaji wa mbegu bora, kuendeleza nishati mbadala, pamoja na kuhamasisha uhifadhi wa vyanzo vya maji.

“Tunatoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya rasilimali za misitu na namna ambavyo jamii inaweza kunufaika kiuchumi bila kuiharibu misitu. Hii ni dhana ya uhifadhi shirikishi,” alisema Solyambingu.

Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani mwaka huu yamebeba kaulimbiu: “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo – Tuwajibike Sasa: Dhibiti Matumizi ya Plastiki”, yakiwa na lengo la kuhamasisha wananchi kuchukua hatua za kulinda mazingira dhidi ya changamoto zinazosababishwa na matumizi mabaya ya plastiki, uharibifu wa misitu na mabadiliko ya tabianchi.

TFS imekuwa miongoni mwa taasisi zilizovutia umati mkubwa wa wananchi katika maonesho hayo kwa ubunifu wa maudhui na huduma mbalimbali, ikiwemo elimu ya upandaji miti, utunzaji wa mbegu, matumizi ya nishati safi na ufugaji wa nyuki kwa tiba na biashara.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...