Na Diana Byera, Simiyu.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Emmanuel Nchimbi, ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi cha miaka minne, ikiwemo kuongezeka kwa mchango wa wizara hiyo katika Pato la Taifa hadi kufikia asilimia 6.

Dr. Nchimbi ameshiriki kongamano kubwa la wafugaji lililofanyika katika Uwanja wa Kabindi, Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, ambapo alijiunga na maelfu ya wafugaji kujadili maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.

Alisema kuwa kwa miaka mingi, Wizara ya Mifugo haikuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa, lakini ndani ya miaka minne pekee, imeonyesha mabadiliko chanya na sasa inachangia asilimia 6 ya Pato la Taifa.

Alibainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na serikali kuongeza bajeti ya wizara hiyo kutoka shilingi bilioni 66 hadi bilioni 400, hatua ambayo imewezesha maboresho mbalimbali katika sekta ya mifugo na uvuvi. Aidha, aliwahakikishia wafugaji kuwa wategemee mabadiliko makubwa zaidi katika sekta hiyo.

“Nakupongeza waziri kwa mabadiliko makubwa sana katika sekta hii, kwa muda mchache umefanya mabadiliko na ubunifu mkubwa na sasa kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya uvuvi hasa upanuaji wa masoko, ufugaji wenye tija na miaka mitano ijayo tutashuhudia mabadiliko makubwa zaidi,” alisema Nchimbi.

Kupitia kongamano hilo, alitaka maamuzi ya mahakama kuhusu wafugaji walioshinda kesi za mifugo yao kukamatwa yatekelezwe haraka na Ofisi ya Waziri Mkuu ili wafugaji hao walipwe fidia.

Aidha, alitoa wito kwa wafugaji kufuata sheria na kujiepusha na migogoro, kwani tayari serikali imemaliza migogoro yote kati ya wakulima na wafugaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Ashatu Kijaji, alisema kuwa mipango ya sasa na mikakati ya wizara hiyo inalenga kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Amesema kuwa kwa sasa, serikali imejipanga kuhakikisha wafugaji wanamiliki ardhi zao na kupanda malisho yao, huku akibainisha kuwa ndani ya miaka 10 ijayo, wizara inalenga kuibua mabilionea 10 kupitia sekta ya ufugaji.

Kongamano hilo limeonesha dhamira ya dhati ya serikali na wadau wa sekta ya mifugo kuibadilisha kuwa chanzo kikubwa cha uchumi na ajira kwa Watanzania.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...