Aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA), Nicodemus Massao, ameanza rasmi safari ya kisiasa kwa kujitosa kuwania ubunge katika Jimbo la Moshi Vijijini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Massao ameonekana leo katika viwanja vya CCM Wilaya ya Moshi Vijijini kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho kuwania ubunge, katika siku ya kwanza ya zoezi la uchukuaji wa fomu za ubunge na udiwani. Zoezi hilo limevutia idadi kubwa ya viongozi wa zamani serikalini, wafanyabiashara, wasomi na makada wa CCM kutoka majimbo mbalimbali nchini.

Jimbo la Moshi Vijijini, ambalo lilikuwa chini ya uongozi wa Prof. Patrick Ndakidemi kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025, limeanza kuvutia wagombea kadhaa, akiwemo Massao ambaye ni kijana msomi na mbobezi katika masuala ya uchumi. Katika siku za karibuni, Massao ameonekana kupata mvuto mkubwa kwa makundi ya vijana na wanawake katika jimbo hilo.

Mbali na kuwa mtaalamu wa uchumi, mipango na biashara za kimataifa, Massao anatajwa kuwa na uzoefu mkubwa katika sekta ya kilimo na biashara. Amefanya kazi katika Wizara ya Kilimo kwenye kitengo cha bajeti na miradi, na pia alikuwa mmoja wa wawezeshaji wa kitaifa katika Programu ya Kilimo (ASDP). Vilevile, aliwahi kuwa Meneja wa Kanda ya Songea, Meneja wa Uendeshaji na Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji katika NFRA.

Kwa sasa, Massao ni Mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Lastanza Financial Services, inayotoa mikopo midogo pamoja na ushauri wa kifedha, biashara na uwekezaji. Kupitia programu yake ya Impact Economy, amesaidia zaidi ya vijana 5,000 nchini kwa kuwapatia ushauri wa kibiashara, hasa katika eneo la kilimo biashara. Aidha, anatajwa kuwa miongoni mwa waasisi wa sera ya vijana katika kilimo pamoja na mradi mkubwa wa vihenge vya kisasa vya kuhifadhia mazao.

Katika ulingo wa siasa, Massao ana historia ya kushika nafasi mbalimbali ndani ya CCM kupitia jumuiya zake, ikiwemo kuwa kiongozi wa UVCCM Chuo Kikuu cha Mzumbe, mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Mkoa wa Morogoro, mjumbe wa kamati ya kata ya Goba (Ubungo) na mlezi wa tawi la UVCCM Mwenge mkoani Kilimanjaro. Pia ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Kata ya Uru Mashariki kupitia Jumuiya ya Wazazi.

Massao pia amewahi kutunukiwa tuzo ya "Champion for Change" kutoka Shirika la Marekani la USAID pamoja na tuzo ya mazingira kutoka taasisi ya Kilimanjaro Environmental Preservation (KEP).

Wasomi wengi kutoka Moshi Vijijini wanaonesha matumaini makubwa kwa Massao kutokana na wasifu wake wa kiuongozi na kitaaluma. Hata hivyo, macho yote sasa yanaelekezwa kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM ili kujua majina yatakayopenya katika orodha ya tatu bora kabla ya kupitishwa mgombea rasmi.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...