Na Pamela Mollel Arusha.

Benki ya NMB imefungua milango kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali nchini kupata mikopo ya mitaji na vifaa muhimu, yakiwemo mitambo, ili kuweza kutekeleza kwa ufanisi tenda wanazoshinda kupitia mfumo wa manunuzi wa serikali, NeST.

Akizungumza katika Kongamano la Tisa la Ununuzi wa Umma jijini Arusha, Meneja Mwandamizi wa Fedha za Biashara (Senior Trade Finance Manager) wa benki hiyo, Jonathan Semzaba, alisema NMB imekuja na suluhisho maalumu kwa changamoto ya ukosefu wa fedha inayowakabili wakandarasi wengi, hususan wazawa na wale kutoka makundi maalum.

“Tunafadhili hadi asilimia 80 ya gharama ya mitambo na vifaa vinavyohitajika ili mkandarasi aweze kuanza kazi mara moja, na baada ya kulipwa na serikali arudishe mkopo huo,” alisema Semzaba.

Alisema lengo ya Benki ya NMB ni kuona wazawa na makundi maalum wengi wanawawezesha kushiriki kikamilifu kwenye zabuni za serikali bila hofu ya ukosefu wa rasilimali.

Alieleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa mfumo wa kidigitali wa NeST, kulikuwepo changamoto nyingi za upotoshaji wa taarifa na mikataba feki.

“Lakini sasa tunaipongeza serikali kwa mfumo huu unaoongeza uwazi, ufanisi na uwajibikaji katika sekta ya ununuzi wa umma,” alisema.

Katika hotuba yake ya kufunga kongamano hilo la siku tano, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, alisema serikali imeweka mazingira mazuri ya kuwawezesha wazawa na makundi maalum kunufaika na miradi ya maendeleo kwa kutenga asilimia 30 ya zabuni zote nchini kwa ajili yao.

“Katika mwaka wa fedha 2023/2024, jumla ya vikundi 119 kutoka makundi maalum vilipata tuzo za zabuni zenye thamani ya Shilingi bilioni 4.02,” alisema Kikwete na kuwataka maafisa maendeleo ya jamii katika halmashauri zote kuwafikia walengwa na kuwapa elimu ya fursa hizo.

Aidha, alikumbusha kuhusu fedha za asilimia 10 za mapato ya ndani ya halmashauri ambazo zinapaswa kukopeshwa bila riba kwa wanawake, vijana na makundi maalum, akisisitiza kuwa hazipaswi kurejeshwa hazina bali ziwafikie walengwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, alisema kongamano hilo liliwaleta pamoja washiriki zaidi ya 1,500 kutoka taasisi mbalimbali, kwa lengo la kujadili na kuboresha mfumo wa manunuzi wa umma nchini.

Simba alifafanua kuwa hadi kufikia Juni 11, 2025, jumla ya wazabuni 38,163 wamesajiliwa kwenye mfumo wa NeST, ambapo 36,377 ni wa ndani na 1,786 ni kutoka nje ya nchi.

Aidha alisema taasisi nunuzi 61,415, zikiwemo taasisi kuu na zile za serikali za mitaa, zimesajiliwa, zikiwa na jumla ya watumiaji 131,202.

"Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, taasisi nunuzi 20,954 zilitangaza mipango ya manunuzi ya mwaka yenye thamani ya zaidi ya Shilingi trilioni 30, na jumla ya zabuni 258,787 zilitangazwa, ambapo 61,174 zilifunguliwa rasmi.

" Tuzo za zabuni 140,494 zilitolewa zenye thamani ya Shilingi trilioni 8.6 kupitia mfumo huo wa kidigitali.

Nae Mkurugenzi wa bodi ya PPRA, Leonada Mwagike alisema kongamano hilo ni kutekeleza dhamira ya dhati ya serikali na wadau kuhakikisha mfumo wa manunuzi wa umma unakuwa jumuishi, wazi na chachu ya maendeleo kwa wazawa na makundi maalum ya kijamii.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...