Visima vitatu vya gesi asilia vinatarajiwa kuchimbwa katika Kitalu cha Mnazi Bay kilichopo Mkoani Mtwara, ikiwa ni miaka kumi (10) tangu kisima cha mwisho kuchimbwa katika Kitalu hicho.

Uchimbaji wa visima hivyo unaotarajiwa kuanza Novemba 2025 unalenga kuongeza uzalishaji wa gesi asilia kutoka Kitalu cha Mnazi Bay kwa zaidi ya futi za ujazo milioni 30 kwa siku.

Akizungumza katika ufunguzi wa warsha kwa wakandarasi watakaoshiriki kazi ya uchimbaji visima hivyo iliyofanyika Juni 26, 2025 Jijini Dar es Salaam, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Bw. Charles Nyangi amesema historia inayokwenda kuandikwa katika Kitalu cha Mnazi Bay ni matokeo ya jitihada zinazofanywa na Serikali kuendeleza sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia.

"Kama ilivyoelezwa, kisima cha mwisho katika Kitalu cha Mnazi Bay kilichimbwa mwaka 2015. Miaka 10 baadae, historia inakwenda kuandikwa kwa kuchimba visima vipya. Kwa hakika, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetekeleza kwa vitendo azma ya kuhakikisha kuwa sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini inaendelea kukua na kuimarika" alisema Nyangi.

Aliongeza kuwa, pamoja na historia ya uchimbaji wa visima vipya, mwaka 2024 Serikali iliweka historia ya kipekee kwa kuwezesha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuongeza ushiriki wake katika Kitalu cha Mnazi Bay kutoka asilimia 20 hadi 40, hatua iliyoongeza nguvu ya kimaamuzi na ushiriki wa TPDC katika Kitalu hicho.

Akizungunzia ushiriki wa watanzania katika mradi huo, Nyangi amesema kuwa PURA imeendelea na itaendelea kuhakikisha kuwa watanzania na watoa huduma wakitanzania wanashiriki kikamilifu katika mradi huu.

"Moja ya majukumu ya PURA ni kuhakikisha watanzania wanashiriki kikamilifu katika miradi ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia inayotekelezwa nchini. PURA imeendelea kufuatilia kwa karibu kila hatua ya utekelezaji wa mradi huu kuhakikisha watanzania wanapata fursa ya kushiriki" alisema Nyangi.

Kwa sasa, Kitalu cha Mnazi Bay kina jumla ya visima vitano (5) vinavyozalisha gesi asilia kwa wastani wa futi za ujazo milioni 90 hadi 100 kwa siku.

Ongezeko la uzalishaji wa gesi asilia unaotarajiwa utawezesha upatikanaji wa gesi zaidi kwa matumizi mbalimbali yakiwemo kuzalisha umeme, matumizi ya viwandani, majumbani na kwenye magari.

Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka PURA, Bw. Charles Nyangi akizungumza wakati wa warsha ya wakandarasi watakaoshiriki mradi wa uchimbaji visima vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay, Mtwara. Warsha hiyo imefanyika Juni 26, 2025 Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wakandarasi na wadau wakichangia mada katika warsha iliyolenga kutoa uelewa wa mradi kwa wakandarasi wataoshiriki mradi wa kuchimba visima vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay, Mtwara. Warsha hiyo iliyoandaliwa na mwendeshaji wa Kitalu cha Mnazi Bay (kampuni ya Maurel et Prom Tanzania) imefanyika Juni 26, 2025 Jijini Dar es Salaam.




Baadhi ya wakandarasi na wadau wakichangia mada katika warsha iliyolenga kutoa uelewa wa mradi kwa wakandarasi wataoshiriki mradi wa kuchimba visima vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay, Mtwara. Warsha hiyo iliyoandaliwa na mwendeshaji wa Kitalu cha Mnazi Bay (kampuni ya Maurel et Prom Tanzania) imefanyika Juni 26, 2025 Jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...