Na - Mwandishi Wetu, TANGA
Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) imempongeza Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Ummy Mwalimu, kwa uchapakazi na uwajibikaji wake wa kuwaletea wananchi maendeleo na namna anavyoilea Jumuiya hiyo muhimu kwa uhai wa Chama.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo wilaya ya Tanga, Bi. Moza Seif, katika Baraza lake la Kikanuni lililokaa Juni 12, 2025 katika Ukumbi wa CCM wilaya ya Tanga ambapo pamoja na mambo mengine, Baraza hilo lilikuwa na ajenda ya kusoma Utekelezaji wa Ilani kwa Madiwani wa Viti Maalum wa Jiji la Tanga.
Bi. Moza amempongeza Mbunge Ummy Mwalimu ambaye amekuwa bega kwa bega na Jumuiya hiyo katika kusukuma gurudumu la maendeleo ndani ya Jiji la Tanga. Katika kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na Mbunge huyo, uongozi wa UWT Tanga ulimpatia Mbunge Ummy Mwalimu Zawadi mbalimbali za Pongezi ambazo zilipokelewa na Bi. Mwanahawa Mwalimu kwa niaba ya Mbunge.
Sambamba na hilo, Madiwani wa Viti Maalum wa Jiji la Tanga walisoma Utekelezaji wa Ilani ambapo kazi nyingi na miradi mingi ya maendeleo imefanyika katika kipindi cha uongozi wao. Aidha, wanachama wameaswa kuwa wamoja kuelekea Uchaguzi Mkuu Mwezi Oktoba, 2025 kwa kuepuka fitna, majungu na makundi.
Katika hatua nyingine, Baraza hilo lilihudhuriwa viongozi mbalimbali wa Chama wakiwemo Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tanga, Meja Mstaafu Hamisi Bakari Mkoba ambaye alikuwa Mgeni Rasmi pamoja na Katibu wa CCM wilaya ya Tanga, Jamal Khimji.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...