Mpwapwa, Dodoma – Juni 28, 2025
WACHIMBAJI wadogo wa madini ya shaba wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma wametakiwa kujiunga katika vikundi ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Mradi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), unaolenga kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini ya kimkakati, ikiwemo shaba.

Wito huo umetolewa na Mhandisi Chacha Megewa kutoka Tume ya Madini, wakati wa utoaji wa elimu kwa wachimbaji katika mgodi wa Minosphere, maarufu kama mgodi wa Majuto, uliopo Kijiji cha Kitati.

Akizungumza na wachimbaji hao, Mhandisi Megewa amesema kuwa ni muhimu wachimbaji kuunda vikundi vya angalau watu watano, ili waweze kufikiwa kwa urahisi kupitia huduma kama mafunzo, uunganishwaji na taasisi za kifedha, pamoja na upatikanaji wa mikopo inayolenga kuongeza tija katika shughuli zao za uchimbaji.

“Uchimbaji salama na wenye tija unahitaji ushirikiano na uratibu mzuri. Kupitia vikundi, wachimbaji watapata nafasi kubwa zaidi ya kunufaika na fursa za kitaifa na kimataifa,” amesisitiza Mhandisi Megewa.

Katika hatua nyingine, Mhandisi huyo amepiga marufuku shughuli za ulipuaji kufanywa na mtu asiye na cheti maalum cha ulipuaji (blasting certificate), akisema hatua hiyo ni hatari kwa usalama wa wachimbaji na jamii inayozunguka migodi.

“Ni kosa kubwa kuhifadhi baruti kwenye makazi ya watu. Baruti ni nyenzo muhimu, lakini isipotunzwa ipasavyo, inaweza kuleta madhara makubwa kwa maisha, mali na mazingira,” amesema, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia maeneo rasmi yaliyoidhinishwa kama stoo au magazini ya kuhifadhi baruti.

Kwa upande wake, Mkaguzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini, Bwana Fahad Mkuu, amewataka wachimbaji kuzingatia usalama mahali pa kazi na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea.

“Wamiliki wa migodi wana jukumu la kuhakikisha wachimbaji wanapata vifaa kinga na mazingira yao ya kazi ni salama. Hii itasaidia kulinda maisha yao na kuongeza ufanisi katika shughuli za uchimbaji,” amesema.

Naye Meneja wa Mgodi wa Minosphere, Bwana Solomon Mhina, ameishukuru Tume ya Madini kwa mafunzo hayo, akiahidi kuyatekeleza maagizo yote yaliyotolewa kwa maslahi ya wachimbaji na maendeleo ya mgodi.

“Tunatambua mchango wa elimu hii kwa ustawi wa mgodi wetu na tutaendelea kushirikiana na Tume ya Madini ili kuhakikisha usalama na tija kwa wachimbaji wetu,” amesema Mhina.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...