Na Said Mwishehe,Michuzi TV
WAJUMBE wa Bodi ya Uongozi wa Wanajeshi Wastaafu (2024) SACCOS LTD na wadau wa maendeleo wamekutana kwa lengo la kuweka mikakati mbalimbali ikiwemo ya kutafuta ufumbuzi wa namna ya kusaidia Wanachama wa SACCOS ambao ni Wanajeshi wastaafu kuanzisha miradi ya uzalishaji mali.
Miradi hiyo inaweza kuanzishwa kwa kuanza na fursa zilizopo ndani ya mali asili ikiwemo aridhi,misitu,ufugaji nyuki ,samaki pamoja na fursa zingine za kimaendeleo zitakazoibuliwa katika mkutano huo wa bodi na wadau hao zote zikilenga kuinua,kuboresha, kustawisha maisha ya wanajeshi wastaafu kiuchumi na kijamii.
Akizungumza leo Juni 30,2025 jijini jijini Dar ea Salaam wakati akifungua mkutano huo maalum ambao pia uliwezesha washiriki kupokea taarifa ya robo mwaka, mgeni rasmi Meja Jenerali (Mstaafu)Sharif Shehe Othman amesema kuwa mkutano huo unaenda kutengeza historia mpya ndani ya SACCOS ya Wanajeshi wastaatu chini ya Sheria ya vyama vya Ushirika.
Amesema pamoja na kwamba mafanikio hayo
yataimarisha Wanachama kiuchumi lakini, watakuwa wezi wa fadhila wasiposema kuwa mafanikio hayo ya ushirika ni tunda linalostawi kupitia kwa Ofisa Ushirika wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.“Tunashukuru kwa ukaribu wenu toka kuanzishwa kwa WANAJESHI WASTAAFU (2024) SACCOS LTD tuendelee kudumisha uhusiano uliopo. “
Akifafanua kuhusu SACCOS amesema uzoefu unaonesha kwamba Wanajeshi wastaafu wana uwezo wa kusisimua uchumi endapo
watapata mwamvuli unaoundwa
kisheria katika kuanzisha miradi ya kiuchumi na kuzalisha mahili kutokana na nidhamu yao iliyojengwa kwenye utumishi, kutokana na
taaluma,fani, ujuzi na uzoefu wao.
“Ingawa hakuna takwimu za kitaalamu zilizothibitisha hayo lakini sote tumeona na kushuhudia uwezo, Utendaji kazi na Ufanisi wa
Jeshi inapopewa jukumu la kushiriki mambo mbali mbali kwenye Mamlaka za kiraia.”
Aidha ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa SACCOS hiyo kuendelea kuhamasisha wanajeshi wastaafu kujiunga na SACCOS hiyo ili kwa pamoja waweze kupanga mipango ikiwemo ya kutumia michango ya wanachama kuwezesha kuwa na fedha kwa ajili ya maendeleo ya wanachama hao.
“Kadri tunavyokuwa wengi na tija itaonekana lakini wanachama wakiwa wachache mzigo utakuwa mkubwa katika kufanikisha mipango ya SACCOS.Hivyo kuna haja ya kuendelea kuhamasisha ili wanajeshi wastaafu wengi zaidi wajiunge na kwa Zanzibar pia ni kuwekwa utaratibu wa kuwafikishia taarifa kwani kuwafikia wastaafu walioko Zanzibar ni rahisi.”
Akiwasilisha taarifa ya robo mwaka Katibu wa SACCOS Ofisa Mteule Daraja la Pili(mstaafu) Johnson Maurice amesema chama cha Ushirika wa akiba na mikopo cha Wanajeshi Wastaafu(2024) SACCOS LTD kilisajiliwa rasmi Agosti 9,2024 na kupewa leseni Septemba 2024 na kwamba mpaka sasa kuna jumla ya wanachama 304.
Kuhusu dira ya SACCOS hiyo amesema ni kuwa miongoni mwa SACCOS bora na madhubuti kiuchumi na kijamii inayotoa ufumbuzi wa changamoto za wanachama katika kutumia taaluma, fani,ujuzi na uzoefu wa wanajeshi wastaafu kuanzisha,kuendesha ,kusimamia na kuendeleza miradi kwa lengo la kusisimua uchumi wao.
Wakati dhima ya SACCOS ni kuinua ,kuboresha na kustawisha maisha ya wanachama wake kiuchumi huku pia akieleza zaidi ameeleza bodi ya uongozi ya wanachama kwa kushirikiana na menejimenti ilianza utekelezaji rasmi wa shughuli za chama Januari 2025.
“Matarajio ya bodi ni kukamilisha malengo ya awali katika kipindi cha mwaka 2025 /26 kwa imani kwamba SACCOS itakuwa imejenga taaswira na uelekeo wake halisi. Bodi na menejimenti inatarajia kujikita kwenye mambo makuu matatu likiwemo kuimarisha chama na wanachama kiuchumi. Pia kuimarisha huduma za kijamii,”amesema Johnson.
Kuhusu hali ya mikopo,amesema hali ya ukuaji wa shughuli za utoaji mikopo kwa wanachama imeendelea kuongezeka hadi kufikia Machi 31,2025 mikopo iliyokuwa imetolewa imefikia Sh.milioni 50.4
Kwa upande wake Luteni Kanali(mstaafu)Isaac Kisahali ambaye ni Katibu wa Kamati ya Mipango ,Uchumi ,Fedha na Uzalishaji Mali katika SACCOS hiyo akitoa taarifa za kamati hiyo amesema kuwa miradi iliyopendekezwa na kamati hiyo ni miradi ya mashamba ya kilimo cha umwagiliaji katika mikoa ya Mbeya,Rukwa,Morogoro ,Dodoma,Tanga na
Manyara.
Pia ufugaji nyuki, ufugaji samaki, kilimo cha SACCOS , kilimo cha mbegu, biashara ya hewa ukaa(Carbon) kampuni ya ulinzi na kampuni ya ujenzi na kukodisha mitambo ya ujenzi.
Kuhusu utekelezaji wa miradi na shughuli za kukuza uchumi ,amesema kwa kuzingatia hali ya uchumi wa SACCOS na uwezo wake wa sasa katika kusimamia miradi kamati inapendekeza utekelezaji wa miradi hiyo ufanyike kwa awamu mbili .
Pamoja na hayo amesema pia kamati imependekeza kuongezwa idadi ya wastaafu watarajiwa pamoja na wastaafu wa zamani wajiunge na SACCOS hiyo kupitia ofisi husika MMJ na Ofisi za mgambo.Pia ufanywe utaratibu kupata takwimu kamili za idadi za wastaafu watarajiwa kila mwaka na chama kiweke mikakati ya usajili idadi maalum iliyopangwa moja kwa moja.










Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...