Na Deogratius Koyanga, Kondoa

Zaidi ya Waraghibishi 30 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa (DC) na Halmashauri ya Mji wa Kondoa (TC) wamepata mafunzo kabambe ya siku nne yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kuongoza mabadiliko katika jamii zao kwa mtazamo wa kijinsia. Mafunzo hayo yamefanyika katika Viwanja vya Riverside, Kondoa Mjini, yakiratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP Mtandao) kwa kushirikiana na The Aga Khan Foundation kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Ireland chini ya mradi wa Tuinuke Pamoja.

Katika mafunzo hayo, Waraghibishi wamefundishwa mbinu za kuibua na kuchambua changamoto zinazowakabili wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na makundi mengine yaliyo pembezoni kwa kutumia mbinu ya ABCD (Asset-Based Community Development) – inayowahimiza kutumia rasilimali zilizopo ndani ya jamii kutatua matatizo yao badala ya kusubiri misaada ya nje.

Akizungumza wakati wa warsha hiyo, Ndg. Deogratius Temba, ambaye ni Mwezeshaji wa Kitaifa katika masuala ya kijinsia na maendeleo ya jamii, alisema mafunzo hayo yamelenga kuimarisha uwezo wa Waraghibishi katika kutoa elimu na kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu kwenye michakato ya maendeleo, hususan mchakato wa bajeti na mipango ya maendeleo ya jamii kwa mtazamo wa kijinsia.


"Kupitia mafunzo haya, Waraghibishi wameelewa kwa kina namna ya kushiriki katika mzunguko wa mchakato wa bajeti ya serikali za mitaa, kuanzia hatua ya uibuaji wa vipaumbele vya kijinsia kupitia mfumo wa O&OD, hadi kuwasilisha mapendekezo kwenye ngazi ya Halmashauri," alisema Ndg. Temba.


Aidha, washiriki walifundishwa jinsi ya kutumia nyenzo mbalimbali za serikali, ikiwemo sera na miongozo ya bajeti, ili kuhakikisha mahitaji ya wanawake na makundi mengine maalum yanazingatiwa katika mipango ya maendeleo.


Kwa upande wake, Bi. Fredina Saidi, mmoja wa wakufunzi wa warsha hiyo, alisema waraghibishi wamefundishwa kutumia mbinu shirikishi kama njia ya kuchambua changamoto na kushauri suluhisho linalojikita kwenye muktadha halisi wa jamii zao.


"Uraghibishi ni kama mwanga unaoangaza giza la changamoto za kijamii. Kupitia mafunzo haya, washiriki wataweza kuchochea majadiliano ya kina katika jamii zao, kufuatilia utekelezaji wa mipango na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika safari ya maendeleo," alisema Bi. Fredina.


Mafunzo haya yamekuja wakati muafaka ambapo serikali za mitaa zinajiandaa kuanza mchakato wa kuandaa bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/26, hivyo kuwapa Waraghibishi nafasi muhimu ya kushiriki kikamilifu kwa niaba ya wananchi, hasa wanawake na makundi yaliyo pembezoni.


Mradi wa Tuinuke Pamoja umekuwa nguzo muhimu ya kuwawezesha wananchi wa ngazi ya jamii kuibua sauti zao, kushiriki kwenye maamuzi na kushinikiza uwajibikaji kwa viongozi, kwa lengo la kujenga jamii jumuishi na yenye usawa wa kijinsia.














Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...