Na Mwandishi wetu

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) tarehe 06 Juni, 2025 amemkabidhi Mkuu wa Majeshi wa kwanza mstaafu Jenerali Mirisho Sam Hagai Sarakikya gari jipya la kisasa aina ya Toyota VXR nyumbani kwake Arumeru nje kidogo ya Jiji la Arusha.

Akiongea muda mfupi kabla ya kumkabidhi gari hilo aina ya Toyota VXR toleo jipya la mwaka 2025 Mhe. Waziri Tax amesema kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa Jenerali Mstaafu Mirisho Sarakikya na Majenerali wengine waliostaafu, ambapo amesema pamoja na kwamba hii ni stahiki yake, lakini stahiki hiyo inatokana na kutambua mchango wa Wakuu wa Majeshi wastaafu katika Ulinzi wa Taifa letu, lakini kipekee mchango wa Jenerali Sarakikya kama Muasisi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ambalo Jenerali Sarakikya alianza nalo hadi lilipobadilishwa, na Jenerali Sarakikya aliyekuwepo na kuweka misingi yote iliyo bora na kuwafanya Wakuu wa Majeshi waliofuata kukuta misingi mazuri ambayo imewezesha Taifa la Tanzania kuwa imara.

Waziri Tax akaongeza kwa kusema “Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan analithamini sana Jeshi lake, anawathamini sana nyinyi waanzilishi, anawathamini sana wote waliochangia katika kuimarisha Ulinzi wa Taifa letu kuhakikisha mipaka ipo salama, uhuru wetu hauteteleki, mapinduzi yetu hayateteleki na Katiba yetu inabaki salama. Kwahiyo kwa kulitambua hilo amewezesha Majenerali wale wote waliokuwa wamefikia muda wa kubadilishiwa magari wabadilishiwe, hivyo naomba nikukabidhi gari hili ili liendelee kukusaidia na kukupa faraja katika maisha yako pamoja na kwamba umestaafu bado ni hazina na uendelee kutusaidia” alisema Mhe. Waziri wa Ulinzi na JKT, Tax.

Awali akimkaribisha Waziri wa Ulinzi na JKT ili akabidhi gari hilo kwa Mkuu wa Majeshi wa Kwanza Mstaafu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe alisema kuwa tukio la kukabidhi gari lililonunuliwa na Serikali, toleo la mwaka 2025 ni stahiki ya Wakuu wa Majeshi Wastaafu kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Ulinzi wa Taifa ya mwaka 1966 pamoja na kanuni zake za mwaka 2015 ambazo zinasema Jenerali wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania baada ya kustaafu atakabidhiwa Gari Jipya la wakati husika.

Naye Mkuu wa Majeshi wa Kwanza, Mstaafu na Mkuu wa Majeshi Muasisi wa JWTZ, Jenerali Sarakikya amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kwa kuendelea kuwakumbuka wastaafu, na pia amemshukuru Waziri wa Ulinzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi kwa kuwa nguzo imara kwao Wastaafu.

Hafla ya kumkabidhi gari kwa Mkuu wa Majeshi Mstaafu wa kwanza, Jenerali Sarakikya imehudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda , Maafisa Wakuu, Maafisa wadogo na Wapiganaji.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...