RAIS wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu na ya Kati Tanzania (TAHLISO),Geofrey Kiliba,akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 10,2025 kuelekea katika maadhimisho ya miaka 21 ya TAHLISO yanayotarajia kufanyika Jumamosi, Juni 14, 2025, katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Na Alex Sonna-DODOMA

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano kubwa la kitaifa la maadhimisho ya miaka 21 ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu na ya Kati Tanzania (TAHLISO), litakalofanyika Jumamosi, tarehe 14 Juni 2025, katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Kongamano hilo linatarajiwa kuwashirikisha wanafunzi zaidi ya 20,000 kutoka vyuo mbalimbali vya elimu ya juu na ya kati nchini, pamoja na viongozi wa Serikali, wadau wa elimu, mashirika ya maendeleo ya vijana na viongozi wa vyuo vikuu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma ,Rais wa TAHLISO), Geofrey Kiliba,amesema kuwa maadhimisho hayo ni fursa ya kujadili mafanikio, changamoto na mwelekeo wa baadaye wa sekta ya elimu, hasa kwa vijana walioko katika ngazi ya elimu ya juu na ya kati.

“TAHLISO imekuwa daraja kati ya wanafunzi na Serikali katika kuhakikisha changamoto zinazowakabili wanavyuo zinapatiwa suluhisho la kudumu kupitia mashauriano na ushirikiano na mamlaka husika,” alisema Kiliba.

Ametaja baadhi ya mafanikio ya TAHLISO katika kipindi cha miaka 21 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004, Kiliba alieleza kuwa yapo katika maeneo kadhaa, ikiwemo kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi vyuoni mwaka hadi mwaka, uboreshaji wa miundombinu ya vyuo, kuimarika kwa huduma za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kuanzishwa kwa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya kati. Aidha, maendeleo ya TEHAMA vyuoni yamechangia kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Katika hatua nyingine, Kiliba alitumia mkutano huo pia kuwatambulisha rasmi viongozi wapya wa TAHLISO kwa mwaka wa uongozi 2025/2026 waliopatikana kupitia Mkutano Mkuu uliofanyika Zanzibar tarehe 5 Aprili 2025 na kuapishwa rasmi Aprili 6, 2025.

Amesema, nafasi ya Rais wa TAHLISO inashikiliwa na Ndg. Geofrey Kiliba, akisaidiwa na Makamu wa Rais, Ndg. Mirahijji Hamisi Mirambo. Ndg. Godfrey Gilagu anaendelea na nafasi ya Katibu Mtendaji, akisaidiwa na Naibu Katibu Mtendaji, Ndg. Muhamad Khamis Mtumwa.

Viongozi wengine ni Katibu wa Seneti, Ndg. Zulekha Afadhali Taib; Mhazini Mkuu, Ndg. Peace Augustine Cornelius; Naibu Mhazini Mkuu, Ndg. Mwanamkuu Jega Bakari; na Katibu wa Ofisi ya Rais, Ndg. Flugence Matata. Pia, jumla ya makamishina 18 wamechaguliwa kuongoza kamisheni mbalimbali za TAHLISO.

Aidha Kiliba aliwataka wanafunzi, wadau wa elimu na wananchi wote kushiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo, ambayo yataanza saa 2:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana, yakibeba kaulimbiu: “TAHLISO ni Yetu Sote.”

“Maadhimisho haya ni ya kihistoria na yanafungua ukurasa mpya wa ushiriki wa wanafunzi katika mabadiliko ya kielimu nchini. Karibuni Dodoma,” alihitimisha.

RAIS wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu na ya Kati Tanzania (TAHLISO),Geofrey Kiliba,akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 10,2025 kuelekea katika maadhimisho ya miaka 21 ya TAHLISO yanayotarajia kufanyika Jumamosi, Juni 14, 2025, katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...