AIRTEL Tanzania imeadhimisha siku ya Ujuzi wa Vijana Duniani kwa mwaka 2025 kwa kuonyesha namna inavyoendelea kuwapa vijana nyenzo za kidijitali na elimu itakayowasaidia kukabiliana na uchumi wa sasa. Kampuni hiyo inasaidia kujenga uelewa wa kidijitali na kuwawezesha vijana kiuchumi nchini Tanzania kupitia mipango ya kibunifu ikiwemo programu kama vile Airtel SMARTWASOMI na Fursa Lab.
Kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho hayo ni ‘Kuwawezesha Vijana Kupitia Ujuzi wa Kidijitali na Akili Mnemba’ ambayo inaenda sambamba na malengo ya Airtel ya kuondoa vikwazo dhidi ya uendelezaji wa ujuzi wa vijana kupitia masuluhisho ya kidijitali. Kwa kutambua kuwa asilimia 60 ya watanzania ni vijana waliochini ya umri wa miaka 25, kampuni hiyo ya mawasiliano iligundua kuwa hatma ya ukuaji wa taifa utategemea zaidi maandalizi ya vijana kuweza kukabiliana na fursa za karne hii ya kidijitali.
Akizungumza kutoka Makao Makuu ya Airtel Tanzania jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Udhibiti wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano, alisema kuwa “Lengo ni kuhakikisha kuwa kila kijana wa kitanzania anapata nyenzo zitakazomsaidia kutumia kipawa chake. Kupitia mradi wa Airtel SMARTWASOMI, tunaondoa kikwazo cha gharama ya kujifunza kwa kuhakikisha maudhui ya mtaala wa elimu yanapatikana bure huku programu ya Fursa Lab ikiwapa vijana pamoja na walimu fursa ya kujenga uwezo kiteknolojia ambao unaendana na mahitaji ya nguvu kazi ya sasa.”
Singano aliongeza kuwa Airtel SMARTWASOMI, ni mradi wa ushirikiano baina ya Airtel Tanzania kupitia Airtel Africa Foundation na Serikali, yenye lengo la kutoa maudhui ya mtaala wa elimu yaliyoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Shule Direct. Jukwaa hilo linarahisisha upatikanaji wa Mafunzo, Masomo na majaribio bila gharama yoyote. Mfumo ambao unatumika kwenye shule zote za serikali mijini na vijijini ili kuboresha ujuzi wa kidijitali kwa wanafunzi.
“Sambamba na hilo, programu ya Fursa Lab, ni mpango ulioanzishwa kwa kushirikiana na Dar Teknohama Business Incubator (DTBi), ambao unaendelea kufanya kazi kama kituo muhimu cha kutoa ujuzi jijini Dar es Salaam. Tangu kuanzishwa kwake, mpango huu umewawezesha maelfu ya vijana na mamia ya walimu kwa kuwapatia ujuzi katika tasnia za ujuzi wa kompyuta, robotics, utengenezaji wa programu za simu, masoko ya kidjitali, na 3D design,” alibainisha.
Singano alifafanua zaidi kuwa, “Katika kusheherekea siku hii muhimu, tunakumbushwa kuwa teknolojia na ushirikiano ni nyenzo zenye nguvu katika kuibua uwezo wa vijana. Ni heshima kubwa kwetu kufanya kazi pamoja na washirika wetu na serikali kuwawezesha watanzania kuwa vinara wa Tanzania ya kesho ya kidijitali.”
Uwekezaji endelevu wa Airtel kupitia majukwaa ya SMARTWASOMI na Fursa Lab yanaunga mkono ajenda ya taifa ya maendeleo na kuchangia katika jitihada za kimataifa za kupanua mafunzo ya kidijitali na uvumbuzi kupitia ushirikiano wa kisekta. Kwa kuangazia siku ya ujuzi wa vijana duniani, Airtel Tanzania inaendelea kuweka kipaumbele kwenye mipango yake ya kimkakati inayolenga kuendeleza uwezeshwaji wa vijana kwa kukuza maendeleo jumuishi ya kidijitali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...