Na Pamela Mollel, Arusha.

Serikali imewataka walimu kuepuka kuchukua mikopo kwenye taasisi zisizo rasmi ambazo zimekuwa zikididimiza uchumi wao badala ya kuwasaidia.

Pia imewataka kuepuka kuchukua kiwango cha mikopo yenye kushusha hadhi za taaluma yao na kutweza utu wao.

Hayo yamesemwa julai 14,2025 na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Karatu, Juma Hokororo wakati akifungua kongamano la 'mwalimu spesho' inayotolewa na benki ya NMB kwa lengo la kuwapatia walimu elimu ya maswala ya kifedha.

Katika kongamano hilo lililohusisha zaidi ya walimu 220 kutoka shule mbalimbali za wilaya ya Karatu, Hokororo amesema kuwa walimu wamekuwa waathirika wakubwa wa mikopo kutoka taasisi zisizo rasmi ambazo zimekuwa zikitoza riba kubwa inayoshindwa kulipika na mwisho kuwafilisi mali walizochuma.

"Mbaya zaidi wengine wanashikilia hadi kadi zenu za benki za ATM ambazo mnaingiziwa mishahara, na Kampuni hizo wanakomba fedha zenu na kuwaacha bila fedha za matumizi"amesema na kuongeza;

"Hii imekuwa ikipelekea walimu wengine kukumbwa na msongo wa mawazo, kushusha weledi na kiwango cha utendaji kazi na zaidi mnaanza kuilaumu serikali kuwa haiwasaidii kutatua matatizo yenu" amesema Hokororo

Amesema kuwa suluhisho la hayo yote ni kuzingatia mikopo kutoka taasisi zilizo rasmi ikiwemo benki ya NMB ambazo Zina riba nafuu na wanaweza kupata msaada kwa dharura yoyote itakayojitokeza.

Hokororo pia amewataka walimu hao kuzingatia Elimu ya matumizi ya kifedha wanayopewa na benki ya NMB kupitia 'mwalimu spesho' ili kutumia fursa ya uwekezaji katika miradi mbalimbali wakiwa kazini kwa ajili ya ustawi wa uchumi wao wa sasa na baadae.

"Mikopo ya NMB imekuwa ikisadia wengi, tumieni hii elimu kuhakikisha mnajishughulisha na miradi mbalimbali mkiwa kazini, hakuna fedha inayotosha kutoka chanzo kimoja cha mshahara pekee bali fugeni, limeni na fungueni biashara kwa ajili ya kuongeza kipato chenu" amesema.

Amewapongeza NMB kwa kuona umuhimu wa kutoa elimu hiyo ya kifedha kwa walimu ili kukuza ustawi wa uchumi wao, lakini pia elimu ya maandalizi ya kustaafu ambayo imekuwa ikiwasumbua sana walimu pindi wanapofikia umri huo.

Akizungumza katika kongamano hilo, meneja mwandamizi wa idara ya wateja binafsi kutoka NMB makao makuu, Ally Ngingite amesema kwa miaka 10 sasa zaidi ya walimu 120,000 wamefikiwa na elimu ya maswala ya kifedha na uwekezaji.

"Leo tuna zaidi ya walimu 220 kutoka karatu ambao tunawapa elimu ya kifedha, uwekezaji, Afya ya akili, mikopo na maandalizi ya kustaafu".

Amesema lengo ni kuwajengea walimu nidhamu ya matumizi ya kifedha, fursa za uwekezaji kwa fedha zao au mikopo lakini pia suluhu la changamoto zao mbalimbali za kifedha kwa ajili ya ustawi wao wa kiuchumi kwa sasa na baadae wakistaafu.

Meneja wa NMB wilaya ya Karatu, Edgar Ninga, amesema kuwa elimu hiyo pia inawasaidia walimu kujua masuluhisho yao ya kifedha za kidigitali zinazotolewa na taasisi hiyo ili waweze kujihudumia mkononi bila na kufuata Ofisi zao.

Mmoja wa walimu kwenye kongamano hilo, Matilda Mathiasi kutoka shule ya Karatu Sekondari amesema kuwa elimu hiyo ni muhimu kwao na itawasaidia kutatua changamoto mbalimbali za kifedha wanazopitia walimu nchini.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...