NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

SHIRIKA la Ndege la Tanzania (ATCL) wamesaini mkataba wa makubaliano na Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) katika uboreshaji wa viwango vya uendeshaji na kuongeza ushindani katika soko la usafiri wa anga la kikanda na kimataifa.

Makubaliano hayo ya maelewano (MoU) yamejikita katika maeneo muhimu ikiwemo huduma za ardhini, matengenezo ya ndege, shughuli za kibiashara, huduma kwa wateja, mafunzo ya wahudumu na usimamizi wa mizigo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo leo Julai 28, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Peter Ulanga amesema ushirikiano huu unaashiria awamu mpya kwa ATCL katika anga ya kimataifa, akisisitiza kuwa makubaliano hayo hayahusu safari au abiria pekee bali pia yanalenga kukuza utaalamu na mifumo thabiti ya ndani kwa maendeleo endelevu ya sekta ya anga.

“Ushirikiano huu unaakisi dhamira ya pamoja: "Tunaunganisha Mataifa," si tu kupitia njia za anga, bali pia kupitia uhamishaji wa ujuzi, kubadilishana maarifa ya kiutendaji na kuendeleza utaalamu endelevu wa ndani." amesema

Amesema kuwa kwa kuzingatia ndege ya mizigo aina ya Boeing 767-300F, Air Tanzania imeweka mizigo kama kipaumbele cha kimkakati. Makubaliano hayo yatarahisisha maendeleo ya utaalamu katika usimamizi wa mizigo kupitia mafunzo ya wafanyakazi, uratibu wa shughuli na kuoanisha viwango na mahitaji ya kimataifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kenya Airways, Allan Kilavuka amesema kuwa ushirikiano huo ni hatua ya mbele katika azma ya kujenga mfumo wa usafiri wa anga wa Afrika uliounganika na wenye uimara.

Amesema ushirikiano katika mafunzo na kubadilishana maarifa hawaimarishi tu mashirika bali pia wanachangia katika maendeleo mapana ya ujuzi na viwango kote katika ukanda huu.

Aidha amesema kuwa makubaliano hayo yatatoa mfumo wa kushirikiana katika shughuli za usafirishaji wa mizigo ikiwa ni pamoja na mafunzo ya wafanyakazi, uratibu wa uendeshaji, na ulinganifu na viwango bora vya kimataifa.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...