• Biashara tatu bora za FinTech zachaguliwa kutoka kwa kumi bora waliofika fainali miongoni mwa maombi 94 yaliyopokelewa

• Washindi watapata zawadi ya kifedha, msaada, fursa ya kuonekana, na nafasi ya kutekeleza suluhisho zao na Benki ya Absa Tanzania

• Hitimisho la safari ya ubunifu na hackathon ya siku 60 kwa ushirikiano na Hindsight Ventures

Benki ya Absa Tanzania kwa kushirikiana na Hindsight Ventures leo imetangaza washindi watatu bora wa shindano la kwanza kabisa la Wazo Challenge Tanzania katika hafla ya Demo Day iliyofanyika kwa shamrashamra jijini Dar es Salaam. Demo Day imehitimisha safari ya ubunifu na ujenzi wa biashara ya siku 60, ikiangazia vipaji bora vya FinTech kutoka Tanzania.

Biashara tatu zilizoshinda – Ghala, Black Swan, na GrupBuy – zimeibuka kutoka kwa kundi la kumi bora waliowasilisha suluhisho zao za kisasa za benki za kidijitali mbele ya jopo la majaji lililojumuisha wataalamu kutoka Benki ya Absa Tanzania na Hindsight Ventures. Startups hizi zimeonyesha ubunifu wa hali ya juu, umuhimu wa suluhisho zao, na uwezo wa kukua, hivyo kupata nafasi ya kutekeleza suluhisho zao kwa ushirikiano na Benki ya Absa Tanzania.

Bw. Sam Mkuyu, Mkuu wa Huduma kwa Wateja na Kidijitali wa Benki ya Absa Tanzania, aliongeza: “Tulibuni Wazo Challenge ili kugundua na kusaidia FinTechs zenye uwezo wa kufanya mageuzi makubwa yanayolingana na mahitaji ya mteja wa kidijitali wa kisasa. Tumefurahishwa na ubunifu mkubwa na uwezo wa washiriki wote. Absa itaendelea kuwa chachu ya uvumbuzi na kushirikiana na vipaji vya teknolojia vya ndani ili kubadilisha sura ya huduma za kibenki nchini Tanzania.”

Mwanzilishi wa Biashara iliyopewa jina la Ghala walioibuka washindi wa kwanza katika shindano la Wazo Challenge, Kalebu Walugalo, wanaojishughulisha na kuwasaidia wafanyabiashara kuuza na kujibu maswali mtandaoni kwa kutumia mfumo wa ‘Akili Unde’ aliwashukuru Benki ya Absa kwani mpango huo umeweza kuwapa fursa ya kuonekana, mafunzo ya wiki nne ya kibiashara na pia zawadi ya pesa.

Wazo Challenge Tanzania, yenye kaulimbiu “Benki ya Baadaye”, iliwaunganisha wabunifu wa FinTech kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ili kuchunguza mada kama vile uzoefu wa mteja, utambulisho wa kidijitali, na bidhaa za kwanza za kidijitali. Washiriki wa fainali walipata fursa ya kufaidika na ushauri, msaada wa kiufundi, mitandao ya kimataifa ya FinTech, na bidhaa za teknolojia zenye thamani ya zaidi ya USD 600,000.

Shindano hili ni hatua muhimu katika mkakati wa ubunifu wa miaka mingi wa Benki ya Absa Tanzania na linathibitisha dhamira ya benki hiyo ya kuwezesha mustakabali wa kidijitali wa Afrika kupitia ushirikiano wa kimkakati na suluhisho jumuishi za kifedha.

Mwanzilishi wa Biashara ya Ghala Kalebu Walugalo akipokea cheti mara baada ya kutangazwa mshindi wa kwanza wa shindano la Wazo Challenge, shindano ambalo liliendesha na  Benki ya Absa kwa kushirikiana na Hindsight Ventures kwa lengo la kugundua na kusaidia FinTechs zenye uwezo wa kufanya mageuzi makubwa yanayolingana na mahitaji ya mteja wa kidijitali wa kisasa

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...