Kamishna Msaidizi Mwandamizi na Meneja wa TEHAMA na Takwimu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Harold Chipanha, amepongeza hatua kubwa za kidigitali zinazotekelezwa na TFS katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) mwaka huu.

Chipanha alitembelea banda la TFS mwishoni mwa wiki hii na kujionea namna wakala huo umefanikiwa kutumia mifumo ya TEHAMA kuboresha huduma kwa wananchi na wadau wa sekta ya misitu, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha taasisi zote za umma zinatumia teknolojia kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Akizungumza baada ya kupata maelezo ya kina kutoka kwa maafisa wa TFS, Chipanha alisema mfumo wa satelite unaotumika kufuatilia moto misituni umeleta mapinduzi makubwa kwa sababu unarahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati, hivyo kusaidia taasisi nyingi zinazohitaji taarifa hizo katika kulinda na kuhifadhi misitu.

“Mfumo huu umewezesha TFS kutoa taarifa kwa wakati sahihi (ontime) na kwa usahihi. Ni jambo kubwa na la kupongezwa kwa sababu linasaidia katika kuzuia uharibifu wa misitu unaotokana na moto,” alisema Chipanha.

Aidha, Chipanha alitembelea pia banda la Utalii Ikolojia na kushuhudia namna programu ya kidigitali ya e-Misitu inavyofanya kazi kwa kuwawezesha wananchi kubook safari za kutembelea vivutio vya misitu kwa njia rahisi kupitia simu zao za mkononi. Alisema kuwa mfumo huo ni kielelezo cha jinsi TFS inavyotekeleza dhamira ya Serikali ya kutoa huduma bora kidigitali.

Mbali na mifumo ya moto na utalii, Chipanha alifurahishwa pia na ubunifu wa TFS katika uzalishaji na uuzaji wa asali ya Misitu Honey ambayo inauzwa kupitia mfumo wa kielektroniki wa Serikali (Government e-Payment Gateway). Akipata maelezo kwenye banda hilo (kama inavyoonekana pichani), Chipanha alishuhudia mfumo wa Honey Traceability System unaotumika kufuatilia ubora wa asali kuanzia kwa mfugaji hadi inapofika sokoni.

“Ubora wa asali hii unahakikiwa hatua kwa hatua. Mfumo huu unatoa uthibitisho wa ubora na unarahisisha kufuatilia mnyororo mzima wa thamani, hii inaongeza imani ya soko na thamani ya bidhaa zetu za misitu,” alisema.

Aidha, Chipanha aliwataka wananchi na wadau kutumia fursa za kidigitali zinazotolewa na TFS ili kujipatia bidhaa na huduma bora kwa njia rahisi na salama.

Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanatarajiwa kufikia kilele chake Julai 13, 2025, huku viongozi mbalimbali wa wizara na taasisi zake wakiendelea kuwasili kushuhudia ubunifu unaoletwa na taasisi za umma kama TFS katika kusukuma mbele agenda ya uchumi wa kidijiti na uhifadhi endelevu.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...