
London / Dar es Salaam, 20 Julai 2025 – Benki ya CRDB imetangazwa kuwa Benki Bora Tanzania, Benki Bora kwa Masuala ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG), na Benki Bora kwa Biashara Ndogo na za Kati (SME) na jarida la kifedha la kimataifa la Euromoney, wakati wa hafla ya kutuza washindi wa Tuzo za Ubora za Euromoney iliyofanyika jijini London Julai 17 2025.
Kutwaa tuzo hizi tatu kubwa katika sekta ya fedha kunathibitisha dhamira ya benki ya kukuza maendeleo jumuishi, uwajibikaji wa kifedha, na maendeleo endelevu, masuala ambayo ambayo yameiongoza Benki ya CRDB kwa miongo mitatu iliyopita.
Tuzo hizo zilipokelewa kwa niaba ya Benki na Bi. Tully Esther Mwambapa, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, katika hafla iliyohudhuriwa na zaidi ya wabobezi 500 wa sekta ya benki na fedha kutoka kote duniani. Bi. Mwambapa aliambatana na maafisa waandamizi wa Benki ya CRDB pamoja na wawakilishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza.
Tuzo hizi tatu zimekuja miezi miwili tu baada ya Benki ya CRDB kutambuliwa na Euromoney kama Benki Bora kwa huduma za benki zinazofata misingi ya Kiislamu nchini Tanzania kupitia huduma zake za CRDB Al Barakah Banking wakati wa tuzo za Euromoney Islamic Finance zilizofanyika Dubai mnamo tarehe 20 Mei 2025.
Tuzo hizi nne kwa pamoja zinaonyesha mtazamo mpana na wa kimkakati wa Benki ya CRDB katika utoaji wa huduma za kifedha unaolenga kuleta mageuzi kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha, kukuza biashara endelevu, na kuwawezesha wananchi katika masoko inayoyahudumia.
Tuzo hizi pia ni za kipekee kwani zinakuja wakati benki inaadhimisha miaka 30 ya uwepo wake sokoni ikisheherekea mchango wake katika kuimarisha masuala ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania tangu mwaka 1996.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hizo, Bi. Mwambapa alisema:
"Heshima hii ya tuzo nne kutoka Euromoney inadhihirisha dhamira ya msingi ya Benki yetu ya kuwa mshirika wa kweli wa maendeleo kwa watu binafsi, wafanyabiashara, na jamii kwa ujumla. Tunapoendelea na kuadhimisha miaka 30 ya Benki ya CRDB, tuzo hizi zinatupa chachu ya kuendelea kusimamia kusudi letu la kuboresha maisha na kuleta mabadiliko chanya ya kudumu katika uendeshaji wetu."
Kutambuliwa kwa Benki ya CRDB kama Benki Bora kwa ESG kunathibitisha nafasi yetu kama kinara wa uwezeshaji wa miradi rafiki kwa mazingira, ujumuishaji wa jamii katika huduma za kifedha, na uwajibikaji wa utawala bora. Benki ya CRDB ilikuwa benki ya kwanza nchini Tanzania kutoa hatifungani ya Kijani “Green Bond” inayolenga kufadhili miradi rafiki kwa mazingira na kuiorodhesha katika Soko la Hisa la Luxembourg (LuxSE), ikiwa miongoni mwa benki chache za biashara Kusini mwa Jangwa la Sahara kufanya hivyo.
Benki ya CRDB pia ndiyo taasisi pekee ya kifedha nchini iliyoidhinishwa na Mfuko wa Hali ya Hewa wa Kimataifa (GCF). Vile vile kupitia taasisi yake ya CRDB Bank Foundation na programu ya Imbeju, benki imeendelea kutoa msaada mkubwa kwa biashara zinazoendeshwa na wanawake na vijana kote katika kanda.

Tuzo ya Benki Bora kwa SME inaonyesha juhudi za benki katika kubuni na kutoa huduma mahsusi kwa biashara ndogo na za kati ambazo ndizo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania wakati tuzo ya jumla ya Benki Bora Tanzania inatambua nafasi ya Benki ya CRDB Bank kama kinara wa ubunifu, mageuzi ya kidigitali, na upanuzi wa huduma za fedha kikanda.
Bi. Tully Esther Mwambapa, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation aliongeza:
"Tunashukuru kupokea tuzo hizi wakati ambao tunaendelea kusimamia vipaumbele vyetu vya kukuza na kulinda biashara yetu huku tukileta athari chanya katika jamii na kujiandaa kwa ajili ya siku za usoni. Tuzo hizi ni alama ya imani ya wateja na wanahisa wetu kwetu, uongozi wenye maono wa bodi na menejimenti, pamoja na kujituma kwa kila mfanyakazi wa Benki ya CRDB."

Benki ya CRDB inapoendelea kutanua huduma zake katika ukanda wa Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla ikiwemo mafanikio ya hivi karibuni ya kuanzisha ofisi zake Dubai, —tuzo hizi kutoka Euromoney zinaimarisha nafasi ya benki kama chombo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...