Na WILLIUM PAUL, SAME.

KAMATI ya Usalama Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro imesisitiza kuwa uamuzi wa kutoa mashamba yenye ukubwa wa hekari 260 yatakayotumiwa kwa muda kwa wakulima wapatao 600 wa Kijiji cha Marwa, ambao mashamba yao yaliathiriwa na mafuriko tangu Mei, umelenga kukabiliana na hatari ya baa la njaa kutokana na wakazi hao kukosa maeneo ya kulima kwa zaidi ya miezi minne.

Hayo yalibainishwa jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni wakati akizungumza na waandishi wa habari waliofika kijijini hapo kufuatilia hatua zilizochukuliwa na serikali baada ya mvua kubwa kusababisha uharibifu wa mali, ikiwa ni pamoja na mashamba.

“Tusingeweza kuwaacha wakulima zaidi ya 600 pamoja na familia zao waendelee kukosa maeneo ya kilimo mkumbuke suala la njaa ni la kiusalama tulitembelea maeneo yote mawili, lile lililoathirika na jingine ambalo wakulima waliomba walitumie kwa muda na baada ya kufanya mkutano na wananchi na kufikia makubaliano, wakulima hao walianza kupewa eneo mbadala kwa mujibu wa makubaliano hayo,” alisema Kasilda.

Hata hivyo, amefafanua kuwa wakati wa kugawa mashamba hayo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Marwa hakushiriki na alikaidi maagizo halali ya serikali.

Aidha, anadaiwa kuunda kikundi cha wafugaji wa jamii ya Kimasai kwa lengo la kuvuruga utekelezaji wa ugawaji huo, huku wakiondoa alama za mipaka ya mashamba yaliyokuwa yameanza kugawiwa na kudaiwa Mwenyekiti huyo ameegemea upande wa wafugaji na kuwabagua wakulima.

Baadhi ya wakulima wameeleza kuwa mwenyekiti huyo ndiye chanzo cha migogoro kati yao na wafugaji, akipinga maagizo ya Mkuu wa Wilaya na kuwatumia wafugaji hao kupinga mchakato wa ugawaji wa mashamba mbadala.

“Tunashangazwa na mwenyekiti wetu ameleta mgawanyiko mkubwa hapa kijijini na sasa ameegemea upande wa wafugaji kwa sababu naye ni mfugaji sisi wakulima tumetengwa na anapinga maagizo ya Mkuu wa Wilaya aliyoyakubali mwenyewe kwenye mkutano wa awali,” alisema mmoja wa wakulima hao.

Waandishi wa habari walijaribu kumtafuta Mwenyekiti wa Kijiji cha Marwa bila mafanikio, licha ya awali kuahidi kufika eneo hilo na wafugaji na hata hivyo, simu zake hazikupatikana na badala yake walifika wakulima ambao waliendelea kueleza changamoto zao.

Kwa sasa Mwenyekiti huyo anakabiliwa na kesi mbalimbali, ikiwemo kesi ya kutishia kuua kwa maneno (Kesi Na. 52 ya mwaka 2025) na kesi nyingine ni Shambulio la kawaida (Na. 54 ya mwaka 2025) inayosikilizwa na Merina Kidesi, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Same.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni amewasihi wananchi hao kuwa watulivu wakati hatua za kushughulikia changamoto hizo zikiendelea.

Kijiji cha Marwa kina wakazi ambao ni wakulima na wafugaji, ambao wanaishi ndani ya Pori tengefu la Same-Ruvu upande wa kata ya Ruvu kwa masharti maalum, ikiwemo kutoanzisha kilimo cha kudumu au maeneo mapya kwa sasa wakati wakisubiri maelekezo ya Kamati Maalum ya Mawaziri Wanane wa Kisekta.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...