MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

SERIKALI imeipongeza Benki ya NMB kwa kuzindua Programu Maalum ya Ujuzi kwa Maendeleo ya Ujasiriamali na Ajira kwa Vijana (SEED), inayolenga kuwaongezea vijana wa Kitanzania Maarifa na Ujuzi wa kujiajiri, pamoja na kuwasaidia mitaji ya kuanzisha na kuendeleza biashara zao wenyewe.

SEED inatekelezwa kwa pamoja kati ya NMB Foundation na Save the Children, ambayo kwa kuanzia itawafikia vijana 200 kutoka Vyuo vya Ufundi jijini Dar es Salaam, vya VETA Dar es Salaam, Kipawa ICT Center na Kigamboni Folk Development College, ambao watapatiwa mafunzo mbalimbali.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa programu hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imekuwa na mpango endelevu wa ujenzi wa Vyuo vya Ufundi katika kila wilaya, hivyo inahitaji uungwaji mkono.

“Ninapozindua programu hii inayoenda kurasimisha ujuzi wa vijana uliopo mtaani, nitumie fursa hii kuwapongeza NMB Foundation na Save the Children sio tu kwa kusaidia vijana watakaonufaika na programu hii, bali pia kuisaidia Serikali kukidhi matumaini ya jamii kwa mtandao wa vyuo hivi.

“Kuwa na vyuo hivi ni jambo moja, lakini kuviwezesha kushughulikia changamoto za ajira zilizopo kwa vijana ambao ni wengi zaidi nchini i jambo jingine, Serikali inahitaji nguvu na bunifu kama hizi kutoka kwa taasisi, mashirika, kampuni na wadau kama hawa.

“Idadi ya vijana 200 mnaoanza nao ni kubwa kwa kuanzia na tunaamini itaamsha ari kwa vijana wengi, nami naahidi Serikali itafuatilia mchakato huu vyuoni kuona mazingira bora ya utekelezwaji wake kwa ustawi na maendeleo ya vijana waliopo huko.

“Matumaini ya wengi ukiwa na Vyuo vya Ufundi vingi, ukipeleka vijana watabadilika watokapo vyuoni, sasa tusipokidhi matumaini hayo, yakiporomoka, itakuwa janga kubwa zaidi, ndio maana Serikali inatoa pongezi na shukrani kwa NMB Foundation kusaidia kukidhi matumaini haya,” alibainisha Prof. Mkenda.

Aliongeza kuwa Tanzania ina vijana na watoto wengi zaidi na takwimu zinaonesha kuwa fursa za ajira hazitoshi na iwapo zitabaki kama zilivyo, itakuwa mkwamo mkubwa na janga la kitaifa na kwamba Serikali inatamani kuona vijana sio tu wanajifunza ufundi, bali wanakua sehemu ya ongezeko la ajira kupitia elimu zao.

Katika uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya NMB Foundation, Bi. Ruth Zaipuna, alisema SEED ni matunda ya maono ya pamoja baina ya benki yake na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, yaliyoangazia namna ya kusaidia vijana kujiendeleza kiuchumi.

Bi. Zaipuna aliishukuru Save the Children kwa kukubali kushirikiana na NMB Foundation, iliyoanzishwa mwaka 2021 kwa lengo la kuchochea juhudi za taasisi yake katika kusaidia jamii inayoizunguka, hasa kwenye Maeneo ya Kimkakati ya Elimu, Afya, Mazingira na Ujasiriamali.

“Leo tuko hapa kuonesha namna Ujasiriamali unavyoenda kutekelezwa kwa vitendo na NMB kupitia NMB Foundation, kuwasaidia Watanzania, hususani Vijana 200 tunaoenda kuanza nao ili kuwa sehemu ya suluhisho la Changamoto ya Ajira nchini, ambako watapatiwa Mafunzo na Elimu ya Usimamizi wa Fedha.

“Kupitia SEED, vijana watapatiwa ujuzi wa Kuanzisha Biashara na Kutambua Fursa Zinazofungamana nazo, Mafunzo ya Usimamizi ya Biashara, pamoja na Mbinu za Usimamizi wa Fedha, ambako vijana wateule tutawawezesha kwa kuwapa mitaji ya vitendea kazi na sio fedha taslimu.

“Hii maana yake ni kuwa, vijana waliopo kwenye Mafunzo ya Teknolojia. tutawapa Vifaa vya Teknolojia kama vile kompyuta, ‘printer’ na ‘photocopy machine’, wanaosomea Useremala tutawapa vifaa vya aina hiyo ya ufundi, halikadhalika kwa vijana wanaojifunza ushonaji, tutawapatia verehani na vinginevyo

“Tunapowashukuru Save the Children kwa kushirikiana nasi, nitumie fursa hii kuyakaribisha mashirika, kampuni na wadau mbalimbali kushirikiana nasi ili kutanua wigo wa kufungua milango ya kukua kielimu, ujuzi na matumaini kwa vijana wa Kitanzania,” alisema Bi. Zaipuna.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa NMB, Foundation, Nelson Karumuna, alisema msukumo wa wazo lililozaa SEED ni takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, iliyoonesha kuwa idadi ya vijana Tanzania ni asilimia 34.5, ambako katika vijana 10, wanne kati yao hawana ajira au fursa za kujikwamua kiuchumi.

“Kwetu sisi NMB Foundation, hiyo sio takwimu tu, bali ni wito wa hatua katika kuwanyanyua vijana hao ambao ndio gurudumu la ukuaji wa taifa, na ndio maana tumebuni programu hii ya SEED ili kuwapatia ujuzi wa vitendo, mitaji ya kuanzisha biashara, na mwongozo wa kuwa wafanyabiashara hodari.

“SEED imeanzishwa ili kupambana na changamoto kubwa kwa vijana kwanye soko la ajira, kwani wengi wanamaliza masomo wakiwa na maarifa ya nadharia pekee, bila kuwa na ujuzi wa vitendo. Na wale waliojiajiri, wanakosa mbinu za kisasa za kijasiriamali pamoja, uelewa mzuri wa masuala ya fedha na ukosefu wa mitaji,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Save the Children, Angela Kauleni, alisema Tanzania, ambayo kimakadirio ina watu karibu milioni 70, inahitaji nguvu za ziada katika uwekezaji na uwezeshaji vijana katika kutimiza ndoto zao za kukua kiuchumi na kielimu.

“Kwa makadirio ya mwaka huu, zaidi ya asilimia 77 ya Watanzania ni vijana walio na umri chini ya miaka 35, huku nusu yao ikiwa ni walio chini ya miaka 18. Kwetu sisi, takwimu hizi sio za kutisha, bali ni fursa ya kujenga taifa lenye nguvu, uvumbuzi na maendeleo.

“Lakini hilo haliwezi kufanikishwa bila kufanya uwekezaji katika ujasiriamali na kuwawezesha vijana, hii ni nafasi ambayo tunapaswa kuiwekea mkazo. Sisi kama wadau, NMB, NMB Foundation, na sisi Save the Children, tunawajibika kuwasaidia vijana kutimiza ndoto zao kwa kushirikiana na Serikali

“Sisi tunaamini kuwa, SEED ni daraja la elimu na ajira, lakini pia ni jibu muhimu kwa sekta kama za kilimo, viwanda vidogo vidogo, TEHAMA na Huduma za Jamii, ambako vijana wanaweza kupata ajira kuanzisha biashara zao na kukua kiuchumi,” alisisitiza Kauleni.











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...