NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
Kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka minne, Benki ya NMB leo imetunukiwa Cheti cha Ithibati ya kutambuliwa kuwa Kinara Katika Mgawanyo wa Kiuchumi Kwenye Suala la Usawa wa Kijinsia Mahali pa Kazi (EDGE Assess), miongoni mwa Taasisi za Fedha barani Afrika.
Cheti hicho kimetolewa na The Edge Certified Foundation ya Uswisi, Taasisi inayoongoza duniani kwa mbinu bora za Tathmini na Udhibiti wa Viwango vya Biashara katika Suala Zima la Usawa wa Kijinsia, ambako mwaka 2022, NMB ilikuwa Benki ya Kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika kutunukiwa.
Akizungumza wakati wa kupokea cheti hicho, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Filbert Mponzi, alisema cheti hicho kinachoitangaza taasisi yake kimataifa, ni cha kujivunia na kwamba Usawa wa Kijinsia kwa benki yake hauishii katika utendaji kazi wa ndani tu, bali pia katika bunifu za masuluhisho yao kwa wateja.
“Cheti cha EDGE Certified Foundation kinaitambua NMB kuwa Kinara wa Sekta ya Kibenki Afrika katika Masuala ya Usawa wa Kijinsia na hii ni mara ya pili tunatupewa. Ni cheti ambacho kinaakisi na kuthibitisha uwepo wa jitihada kubwa za kuzingatia Usawa Kijinsi Mahali pa Kazi.
“Kwetu sisi NMB, Usawa wa Kijinsia hatuuangalii tu katika utendaji kazi ndani ya taassisi yetu, bali pia katika aina ya bunifu za masuluhisho yetu yanayozingatia Mpango Mkakati hupo, uthibitisho ukiwa ni pamoja na Hatifungani ya JASIRI tuliyoingiza sokoni na kuvuna mabilioni ya shilingi za Kitanzania.
“Hatifungani ya JASIRI iliuzwa kwa zaidi ya Sh. Bilioni 70, ambazo zilielekezwa katika mikopo ya riba nafuu kwenye biashara zinazoongozwa ama kugusa maisha ya wanawake, ambako mikopo zaidi ya 3,200 ilitolewa na pesa zote hizo (Sh. Bil. 70) zimekopeshwa tayari.
“Kwa ujumla, katika miaka michache tumeendelea kuongeza uwiano miongoni mwa wafanyakazi, kufikia Desemba 31, 2024, NMB ilikuwa na jumla ya waajiriwa 5,204 kutoka waajiriwa 3,544 tuliokuwa nao kufikia Desemba ya mwaka 2022.
“Mgawanyo wa kijinisa miongoni mwa wafanyakazi wetu kwa sasa ni waajiriwa wanaume ni 2,564 sawa na asilimia 49.26 na waajiriwa wanawake wako 2,640 sawa na asilimia 50.74,” alibainisha Mponzi katika hotuba yake wakati wa hafla hiyo na kuongeza:
“Utafiti unaonesha kuwa taasisi zenye Usawa wa Kijinsia, ndizo zinazopata mafanikio makubwa zaidi, NMB chini ya Afisa Mtendaji Mkuu, Bi. Ruth Zaipuna ni uthibitisho na kielelezo cha hilo, mafanikio ya benki ni makubwa pale idadi ya wafanyakazi inapoelekea kulingana,” alisema Mponzi.
Aliongeza kuwa NMB itajikita zaidi katika ubunifu wa masuluhisho ya kutatua changamoto za makundi yote hasa wanawake, na kwamba baaada ya kupokea cheti hicho, wanatamani kuwa chachu ya Usawa wa Kijinsia Tanzania, huku akitaka taasisi mbalimbali zijifunza kwao namna ya kujenga usawa mahali pa kazi.
Akikabidhi cheti hicho, Meneja wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) Kanda ya Afrika Mashariki, Samuel Ng’ang’a, aliipongeza NMB kwa kuendelea kuamini katika Usawa wa Kijinsia na kwamba mgawanyo huo una faida nyingi Kibiashara na Kiuchumi kwa ukuaji wa taasisi kitaifa na kimataifa.
Akiunga mkono kauli ya Mponzi, Ng’ang’a alibainisha kuwaUsawa wa Kijinsia Mahali pa Kazi unachochea ubunifu, ukuaji wa kiuchumi na utulivu wa kifedha na kwamba kinachofanywa na NMB katika hilo ni alama ya kudumu na mbegu bora ya mafanikio kwa kwa taasisi.
“Mafanikio haya yanayowapa tuzo ya pili katika Masuala ya Usawa wa Kijinsia Mahala pa Kazi, yanaakisi maendeleo endelevu katika ngazi zote za usimamizi na uboreshaji wa mitazamo ya wafanyakazi na kujenga imani yao thabiti juu ya benki hii na malengo yake katika Nyanja ya Mgawanyo wa Kiuchumi,” alisema Ng’ang’a.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Rasirimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuiel Akonaay, aliishukuiru EDGE Certisified Foundation kwa cheti hicho na kwamba Usawa wa Kijinsia ni miongoni wa vipaumebele vya benki yake, kama walivyothibitisha kupitia program mbalimbali na masuluhisho yao kihuduma.
Akonaay alisisitiza kuwa wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wateja wao katika kufikia Malengo ya Jamii ya Usawa Kijinsia katika kila Nyanja, huku akiwashukuru wafanyakazi, wateja pamoja na wadau wa NMB kwa kuwa sehemu ya utambuzi huo.
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...