Na: Calvin Edward Gwabara – Dar es Salaam.
Imebainishwa kuwa Ofisi ya
Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini (OCPD) ndio nguzo muhimu inayoshikilia
Uandishi, Urekebu na Ufasili wa sheria Kuu na sheria Ndogo nchini kwakuwa bila
ofisi hiyo hakuna sheria ya nchi inayokwenda kutungwa bungeni.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akiangalia sehemu ya vitabu vilivyoandaliwa na OCPD kwaajili ya matumizi ya kazi za ufasili na urekebu. |
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati akizungumza na Waandishi wa
habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini alipotembelea banda la OCPD kwenye
maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya SABASABA yanayoendelea kwenye viwanja vya
Mwl Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam.
“Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa
Sheria nchini ni Ofisi muhimu sana katika mchakato mzima wa utunzi, Urekebu na
Ufasili wa sheria za nchi, bila Ofisi hii hakuna sheria ambayo itakwenda
bungeni kutungwa, bila ofisi hii hakuna sheria ambayo itafanyiwa Urekebu wala
marekebisho lakini pia bila ofisi hii hakuna sheria ndogo ambayo itatungwa
hivyo ni Ofisi muhimu sana katika mchakato mzima wa sheria nchini” Alifafanua
Mhe. Dkt. Ndumbaro.
Aliongeza” Ikifa Ofisi hii maana
yake Mahakama itapata shida katika utoaji wa haki maana ndiyo Ofisi ambayo inatuambia
sheria sahihi ni ipi na ya toleo la mwaka fulani lakini pia sheria ipi si
sahihi, lakini kwa sasa wanafanya kazi nzuri sana ya kufasili sheria zetu zote
kutoka katika lugha ya Kiingereza kwenda katika lugha yetu ya Kiswahili”.
Amesema kwa taarifa alizonazo
hadi kufikia tarehe 30 mwezi wa sita tayari OCPD ilikuwa imeshafanya ufasili wa
sheria 300 kati ya sheria 446 na kwamba Serikali katika mwaka huu wa fedha
wametenga fedha za kutosha kwa Ofisi hiyo ili iweze kukamilisha ufasili wa
sheria zote za nchi Watanzania waweze kuzielewa.
Waziri huyo wa Katiba na Sheria
amesema Ofisi hiyo ya Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini ni Ofisi muhimu katika
mchakato mzima wa uchakataji wa sheria za nchi na inasaidia Bunge kwenye
kuchakata miswada kuwa sheria kamili zinazozingatia misingi yote muhimu ya
utungwaji wa sheria.
Awali akitoa maelezo kwa Waziri
bandani hapo Mwandishi wa sheria kutoka OCPD Bwana Philemon Mrosso amemueleza Waziri
huyo kuwa Ofisi hiyo ipo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha zoezi la ufasili
wa sheria zilizobakia sambamba na kanuni zake ili ziweze kutoka kabla ya mwezi
octoba mwaka huu kwa matumizi.
“Mhe. Waziri naomba nikujulishe
kuwa ofisi yetu inashiriki maonesho haya kuweza kutoa elimu kwa watanzania na
wadau wote wa sheria kuhusu mchato mzima wa utungwaji wa sheria lakini pia kuwafahamisha
kuhusu majukumu ya Ofisi hii ili wanapohitaji msaada katika masuala yaliyo
ndani ya mamlaka ya Ofisi yetu waweze kutufikia kirahisi na kupata msaada”
Alieleza Mrosso.
Aidha ameongeza kuwa wanapokea
maoni mbalimbali ya Wananchi na wadau kuhusu sheria za nchi na kuwaelekeza njia
sahihi za kufikisha mawazo yao ikiwemo nafasi yao kama jamii katika utungwaji
wa sheria za nchi katika maeneo mbalimbali kupitia wawakilishi wao ndani ya
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwandishi wa sheria kutoka OCPD Bwana Philemon Mrosso akimkabidhi zawadi Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Ndumbaro |
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akisaini kitabu cha wageni wanaotembelea banda hilo la OCPD.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akijisajili kidigitali kwenye mfumo maalumu wa wageni kwenye banda hilo. |
![]() |
Wanafunzi wakijisajili baada ya kupata maelezo na elimu kwenye banda la OCPD |
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...