
Na John Mapepele
Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia eneo la Afya, Prof. Tumaini Nagu amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kote nchini kuendelea kuzingatia taaluma na kufanya kazi kwa bidii ikiwa ni kusherekea mafanikio makubwa ambayo yamepatikana katika Sekta ya Afya Msingi yaliyofanywa na Serikali kwa kipindi cha miaka minne cha Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Prof. Nagu ameyasema hayo leo wakati akitoa neno la utangulizi katika Mkutano Mkuu wa Waganga wa Wakuu wa Mikoa na Halmashauri unaofanyika kwa siku tatu katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya kikwete Jijini Dodoma ulioanza leo.

Prof. Nagu amempongeza Mhe Rais kwa maboresho makubwa aliyoyafanya katika kipindi kifupi cha uongozi wake na kuwataka madaktari hao kusimamia vizuri uwekezaji huo ili wananchi wa chini waweze kunufaika na huduma za afya zinazotolewa na Serikali kote nchini.
“Ndugu zangu sote tunatambua uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwa ajili ya watu wake, hususani katika Sekta ya Afya, kwa ngazi ya Afya ya Msingi ambako ndipo wananchi wengi walipo kwani zaidi ya 95% ya Wananchi ndipo wanapopata huduma za afya” amefafanua, Prof. Nagu.

Aidha, amesema malengo ya mkutano huo ni kujadiliana mambo mbalimbali ikiwepo kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma za afya katika ngazi ya msingi, kuboresha namna za usimamizi wa rasilimali zilizopo vituoni pamoja na miundombinu, kuweka Mikakati ya pamoja kuboresha uratibu katika ngazi ya Taifa, Mikoa na Halmashauri na kutekeleza mipango ya afya.
Naye, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema Waganga wa Wakuu wa Mikoa na Halmashauri ni wadau muhimu sana katika kuandaa Sera mbalimbali za afya kwani wao ndio watekelezaji wakuu wa Sera hizo hivyo maoni yao ni muhimu sana.
Mkutano huo mwenye kauli mbinu ya “Wajibu wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri katika kuimarisha ubora wa huduma za afya kuelekea bima ya afya kwa wote” unatarajiwa kumfungulia na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hapo kesho.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...