Na Mwandishi Wetu, Ndola
Serikali ya Tanzania, kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), imeweka msingi wa suluhisho la kudumu kukabiliana na changamoto ya uingizwaji wa mazao ya misitu kutoka Zambia bila vibali halali.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kikao kazi maalumu kilichofanyika leo Julai 7, 2025, pembeni mwa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Zambia (ZITFT) yanayoendelea mjini Ndola.
Ujumbe wa Tanzania, ukiongozwa na Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayeshughulikia Masoko na Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Misitu, DCC Salehe Beleko, ulikutana na Mkurugenzi wa Idara ya Misitu Zambia, Bw. Sitwala Wamunyima na timu yake, kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo.
Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Beleko alisema mazungumzo hayo yamelenga kuondoa changamoto ya muda mrefu ambapo shehena za mazao ya misitu kutoka Zambia zimekuwa zikikamatwa Tanzania zikiwa na nyaraka zinazodaiwa kutotambuliwa na mamlaka husika za Zambia.
“Tumeona ni muhimu kuweka mfumo wa mawasiliano na ufuatiliaji wa pamoja ili kuondoa usumbufu kwa wafanyabiashara na kupunguza gharama za ufuatiliaji wa mizigo inayokwama mipakani,” alisema Beleko.
Kwa upande wake, Bw. Wamunyima alikiri kuwa Zambia bado ina safari ndefu katika kuboresha mifumo ya usimamizi wa misitu, na ameahidi kwamba ifikapo Desemba mwaka huu nchi hiyo itakuwa na mfumo rasmi wa kutoa vibali unaotambulika kimataifa na kushirikishwa na mamlaka za Tanzania.
“Nchi yetu bado ni changa katika mifumo ya usimamizi wa misitu. Tunahitaji kujifunza kutoka Tanzania, hususan katika uanzishaji wa mashamba ya miti, ufugaji nyuki na utoaji wa vibali kwa njia ya kidijitali,” alisema Wamunyima.
Katika hatua nyingine, Makamu Mkuu wa Chuo cha Misitu Zambia, Bw. Shawa Patrice, alisema wanatarajia kujifunza kuhusu mtaala wa Chuo cha Misitu Tanzania (FTI) ili kuboresha mitaala yao na kuendana na mahitaji ya soko la ajira la sasa.
Pamoja na kikao hicho, ujumbe wa TFS pia ulitembelea Kampuni ya Umma ya Upandaji na Uzalishaji Mazao ya Misitu Zambia (ZAFFICO) na kufanya mazungumzo ya kushirikiana katika kubadilishana ujuzi na malighafi za kibiashara.
Maonesho ya ZITFT 2025 yalizinduliwa Julai 5 na Waziri wa Mipango na Fedha wa Zambia, Dk. Situmbeko Musokotwane, kwa niaba ya Rais Hakainde Hichilema, na yanatarajiwa kuvutia washiriki kutoka ndani na nje ya Afrika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...