Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kuboresha Ushauri kwa Taasisi za Umma wakati wa kuingia mikataba mbalimbali ili kuwa na Mikataba iliyobora na kutimiza malengo ya Serikali ya kuwa na mikataba inayotekelezwa vizuri na kuwanufaisha Wananchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno tarehe 7 Julai, 2025 katika Maonesho ya Kimataifa ya 49 ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba Jijini Dar es Salaam.
"Tunaendelea kuzipa ushauri Taasisi za Umma ili kuwa na ubora wa mikataba pia kuhakikisha kwamba utekelezaji wa Mikataba hiyo unafanyika kwa mujibu wa Makubaliano".* Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Aidha, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inayatumia maonesho hayo katika kutoa Ushauri wa Kisheria, Kushughulikia Malalamiko, Utatuzi wa Migogoro na Elimu ya Sheria hususani sheria zilizofanyiwa Urekebu toleo la Mwaka 2023 zilizoanza kutumika Julai 1, 2025.
"Sheria zilizofanyiwa urekebu zimezinduliwa na zimeanza kutumika na kitu kizuri ni kuwa kati ya sheria 446 sheria 300 zinapatikana kwa lugha ya kiswahili".* Ameeleza Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Katika hatua nyingine Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitembelea mabanda ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria pamoja na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, kuona shughuli zinazotekelezwa na Taasisi hizo katika maonesho hayo.
Maonesho ya Sabasaba 2025 yamezinduliwa rasmi leo tarehe 7 Julai, 2025 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambapo maonesho yanatarajiwa kumalizika tarehe 13 Julai, 2025.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...