Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, wametangaza kuanza rasmi kwa shindano la uandishi wa insha kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 26 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma za Televisheni wa TBC, Bi. Happiness Ngasala, amesema shindano hilo lina lengo la kuwahamasisha vijana kuenzi mchango wa Mwalimu Nyerere kwa njia ya maandishi na tafakuri ya kina kuhusu juhudi zake katika kulijenga taifa.
“Tunataka wanafunzi waandike insha zitakazoonyesha uelewa wao kuhusu mchango wa Mwalimu Nyerere katika mapambano dhidi ya ujinga, maradhi na umasikini,” amesema Bi. Ngasala.
Shindano hili litahusisha wanafunzi wote kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, likiwa na mada kuu zinazolenga kuangazia falsafa ya Mwalimu Nyerere na maono yake katika maendeleo ya taifa. Lugha zitakazotumika ni Kiswahili na Kiingereza, na washindi watano bora watazawadiwa kompyuta mpakato na fedha taslimu.
Aidha, Bi. Ngasala amebainisha kuwa kutakuwa na uchunguzi maalum wa kuhakikisha uhalisia wa kazi zinazowasilishwa, huku akionya kuwa matumizi ya teknolojia ya akili bandia (AI) kughushi insha ni kosa litakalosababisha mshiriki kuondolewa kwenye shindano.
Shindano limezinduliwa leo, Julai 22, 2025, na litahitimishwa rasmi Oktoba 14, 2025 – siku ya kumbukizi ya kifo cha Mwalimu Nyerere. Kilele cha maadhimisho hayo kitasindikizwa na mbio za pole za “Mwalimu Nyerere Marathon.”
Wanafunzi wa shule zote za sekondari nchini wanahimizwa kushiriki kwa wingi ili kuenzi urithi wa Baba wa Taifa. Utaratibu rasmi wa ushiriki utatangazwa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ya TBC na Wizara husika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...