Na Karama Kenyunko, Michuzi Tv

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) wamesaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya bima na masoko ya mitaji nchini.

Pia Taasisi hizo mbili zitashirikiana pamoja na ujumuishaji wa kifedha ili kuimarisha uwekezaji katika sekta ya bima.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt Baghayo Saqware, ameeleza kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuhakikisha sekta ya bima inakuwa thabiti, shindani na jumuishi, sambamba na kuendana na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita iliyochini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukuza uchumi kupitia sekta binafsi.

"Ushirikiano huu utasaidia kuyafanya makampuni ya bima kuwa imara na stahimilivu, na hivyo wananchi kuendelea kupata kinga bora kwa mali, afya na uwekezaji wao, huku pia ukiboresha mifumo ya taarifa na kuwezesha kampuni hizo kuongeza mitaji kupitia soko la hisa,"amesema dkt Saqware

Amongeza kuwa makubaliano hayo ni fursa ya kuunganisha nguvu katika kukuza bidhaa bunifu za kifedha kama vile bima zinazoweza kuorodheshwa sokoni, pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya kifedha.

“TIRA inaamini mafanikio ya sekta ya bima hayawezi kutenganishwa na uimara wa masoko ya hisa ushirikiano huu unalenga kuimarisha mifumo ya taarifa, uwazi na uwajibikaji katika sekta hizi mbili muhimu,” amesema Sakware.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela, amesisitiza kuwa makubaliano hayo ni dira ya kimkakati ya kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kwa watanzania wote.

Amesema hatua hiyo inalenga kuboresha uwazi katika sekta za kifedha, kuongeza nidhamu ya fedha kwa taasisi, na kuchochea kasi ya mabadiliko ya kiuchumi, sambamba na kuhamasisha kampuni za bima kuwekeza kwenye soko la hisa ili kujenga uchumi imara na endelevu.

“Tutahamasisha kampuni za bima kutumia fursa ya soko la hisa kwa ajili ya kupata mtaji, kuimarisha utawala bora, na kukuza uelewa wa jamii juu ya uwekezaji,” amesema.

Makubaliano hayo yanajumuisha maeneo kadhaa ya ushirikiano ambayo ni kuandaa kampeni za elimu ya fedha kwa wananchi na wafanyabiashara wadogo, kuendesha mafunzo ya pamoja kwa kampuni za bima kuhusu mchakato wa kuorodheshwa DSE (IPO), na kuanzisha mikutano ya kila mwaka kati ya taasisi hizo mbili kwa lengo la kubadilishana uzoefu na taarifa.

Sekta ya masoko ya mitaji imeelezwa kuwa ina nafasi muhimu katika kusaidia kampuni za bima kupata mtaji wa muda mrefu, kuongeza uwazi wa kifedha na kuimarisha usimamizi wa hatari. Vilevile, makubaliano hayo yameainisha mpango wa pamoja wa kuandaa matukio kama siku ya Bima ya Kila Mwaka, ripoti za pamoja na mikutano ya wakurugenzi wa sekta husika.

Katika hotuba zao viongozi wa taasisi zote mbili walisisitiza kuwa makubaliano hayo si mwisho, bali mwanzo wa sura mpya ya ushirikiano wa kimkakati kwa maendeleo jumuishi na endelevu ya sekta ya fedha nchini Tanzania.

Viongozi hao wamesema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 na kujenga mfumo imara wa kifedha, huku wakihimiza wananchi na taasisi za bima kuendelea kutumia huduma za bima kwa kuwa sekta hiyo inasimamiwa ipasavyo.




Kamishna Bima Tanzania,  Baghayo Saqware (Kulia) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Peter Nalitolela wakibadirishana nyaraka baada ya kusaini  mkataba wa makubaliano kati ya hizo sekta mbili. Hafla ya kutiliana saini kwa makubaliano hayo imefanyika leo Julai 31, 2025 jijini Dar es Salaam

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...