Kampuni ya usafiri wa mtandaoni Bolt Tanzania kwa pamoja na Chama cha Madereva Mtandaoni Tanzania imezindua rasmi programu ya mafunzo ya siku 10 kwa madereva wake wa jiji la Dar es Salaam. Mafunzo hayo yalianza jana katika ghorofa ya tatu ya jengo la Tropical na yataendelea hadi Agosti 8.

Mpango huu unajumuisha vipengele vitatu muhimu: Mafunzo na vyeti vya Usafiri wa Umma (PSV) kwa kushirikiana na Taasisi ya Usafirishaji Tanzania (NIT); Moduli ya Bolt Best Practices inayolenga kukuza huduma bora na kujenga uaminifu kati ya dereva na mteja; na Mafunzo ya Misingi ya Kukabiliana na Dharura Barabarani, yatakayowawezesha madereva kushughulikia matukio kwa haraka na kwa usalama.

Huu ni mwendelezo wa dhamira ya Bolt kuhakikisha usalama, utiifu wa sheria, na uwezeshaji wa madereva nchini. Kupitia mafunzo haya, Bolt inalenga kuongeza taaluma ya madereva, kuwapa ujuzi wa kukabiliana na dharura, na kuwahamasisha kufuata sheria za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA).

Utafiti wa hivi karibuni uliochapishwa na Tanzania Journal of Development Studies umebaini kuwa "ubora wa huduma, muda wa huduma, na mienendo ya kitaaluma ya madereva ndizo sababu kuu zinazowaridhisha wateja wa usafiri wa mtandaoni nchini Tanzania." Aidha, utafiti mwingine unaonyesha kuwa "asilimia zaidi ya 65 ya abiria huzingatia zaidi tabia ya madereva iliyo na heshima na weledi kama kigezo cha kuchagua jukwaa la usafiri mara kwa mara."

Dimmy Kanyankole, Meneja Mkuu wa Bolt Tanzania, amesema: “Matokeo haya yanaonesha umuhimu wa kuwekeza kwa kina katika taaluma ya madereva na uwezo wao wa kuwahudumia wateja kwa weledi – jambo ambalo Bolt na TODA wanalitekeleza moja kwa moja kupitia mpango huu.”

“Kupitia mafunzo haya ya darasani na kwa vitendo ya siku 10 kwa kushirikiana na TODA, madereva wanapata fursa ya kueleza changamoto zao na kujifunza mbinu bora za kushughulika na abiria wasumbufu pamoja na matukio yasiyotarajiwa barabarani,” aliongeza.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...